Na Stephen Jackson, Kongwa.
Naibu waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa Nchini Namibia Mhe. Jennelly Matundu , Leo Tarehe 2 Machi, 2022 , Amefanya ziara Wilayani Kongwa.
Katika ziara hiyo amekutana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel na kufanya mazungumzo na akinamama kadhaa wanaodai kupoteza watoto wao miaka kadhaa iliyopita.
Inadaiwa kuwa Watoto hao walichukuliwa na kupelekwa nchini Namibia kwa lengo la kupelekwa shule na hawakuweza kurejeshwa hadi sasa.
Wakielezea kwa masikitiko, akina mama hao walieleza kuwa wamepoteza matumaini ya kuwapata watoto wao kwani hawana mawasiliano nao kwa muda mrefu, hivyo wameiomba serikali ya Namibia kufuatilia Jambo hilo.
Akizungumza kwa masikitiko, Mara baada ya kupokea maelezo hayo, Mhe. Jennelly Matundu, amesema kuwa maelezo hayo yanaamsha simanzi, hivyo ameahidi kuwa serikali ya nchi yake itayafanyia kazi na familia hizo zitapatiwa mrejesho kupitia ubalozi wa Namibia Nchini hapa.
Baada ya mazungumzo hayo ya muda mrefu, Naibu huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Namibia, ametembelea katika makumbusho ya iliyokuwa kambi ya Wapigania Uhuru ambayo kawa sasa ni Shule ya Sekondari Kongwa, ambapo alipokelewa na uongozi wa shule hiyo Kisha kuongea na wanafunzi na kuhitimisha ziara hiyo kwa kutembelea Makaburi ya Mashujaa wa Namibia yaliyopo kitongoji cha Morisheni mjini Kongwa.
Mambo mengine yaliyozungumziwa ni pamoja na mpango wa kuboresha miundombinu katika maeneo hayo ya kihistoria ili kuwa moja ya sehemu zitakazovutia watalii.
Mhe. Matundu alifuatana na Balozi wa nchi hiyo hapa nchini Mhe. Lebbius Tangeni Tobias na Maafisa wengine kutoka Namibia ambapo Kamati kuu ya ulinzi na Usalama ya Wilaya, ya Kongwa, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila, viongozi wa CCM (W), kaimu Mkurugenzi Mtendaji (W) na baadhi ya Maofisa kutoka Halmashauri ya Kongwa walihudhuria.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.