Kituo cha Afya Ugogoni kimeanza kutoa huduma ya upasuaji, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Ndg. Dkt. Suleiman Serera amezindua huduma leo tarehe 11 Agosti, 2020.
Akizungumza na Wananchi, Ndg. Dkt. Serera amesema pamoja kwamba Kituo kilianza lakini leo tumezindua huduma za upasuaji kwa ajili ya kinamama kwa kuanzia, lakini jengo hili ni pamoja na upasuaji mbalimbali ambao tunatarji kuona.
Dkt. Serera ameipongeza kamati ya ujenzi, kwani yeye binafsi ameingia na ameona majengo na ameridhia ubora uliopo. Pia, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Ugogoni.
Aidha, Dkt. Serera amesema Mhe. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anaelewa nini kinatakiwa kufanyike, na sisi wote tumeona katika risala iliyosomwa kwamba “bila afya madhubuti huo uchumi wa viwanda hauwezi kukamilika” ili tuwe na viwanda lazima watu wetu wawe na afya nje, tuwe na afya ya akili kwa maana ya watoto wetu wanaozaliwa, na bila afya hatuwezi kufanya lolote na bila afya tusingeweza kuwepo katika uzinduzi huu leo.
Pia, Dkt. Serera amesema nchi yetu ya Tanzania imeridhia kutekeleza Mpango Mkakati wa Afya wa nne, ambao unajulikana kama “HSSP IV” wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga. Hali halisi kwa sasa hivi, iliyopo katika nchi yetu, vifo vya akina mama tunavyo vifo 556 kati ya walio hai 100,000 na tuna vifo vya watoto wachanga 25 kwa kila vizazi hai 1,000. Tatizo hili ni kubwa, lakini kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa vifo vitokanavyo na uzazi ni 43 100,000 na watoto 25 kati ya 1,000. Sasa hapa utaona kwamba lengo la Serikali wakati wote imekuwa ni kupunguza vifo vya uzazi kutoka 556 kati ya 100,000 hadi kufikia vifo 292 katika kila vizazi 100,000 ifikapo mwaka 2020, ambao huu unaishia. Lakini pia, kupunguza vifo vya watoto 25 katika kila watoto 1,000 hadi kufikia 16 katika kila watoto 1,000 ifikapo mwaka 2020.
Dkt. Serera amesema “Naamini kwamba vifo hivi vitapungua kwa sababu leo tumeweza kuzindua jengo hili na niwahakikishie kwamba nimeingia na umeshafanyika upasuaji mmoja, na tumemuona mgonjwa, anaendelea vizuri, amejifungua pale, mtoto tumemuona mzuri na ana afya njema kabisa. Kwa hiyo niwasihi, baada ya kuwapongeza madaktari wetu waliofanya upasuaji huo, tuendelee kuwaombea mama na mtoto waendelee kuimarika zaidi ili wakitoka wakawe mashuhuda bora wa Kituo chetu hiki cha Afya kwa upasuaji uliofanyika.”
Aidha, Dkt. Serera amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano imejikita katika kuimarisha uboreshaji wa mazingira ya kutoa huduma bora za afya, zikiwemo huduma za afya ya uzazi, na mtoto. Lakini ili kufikia lengo, lililokusudiwa Serikali imekuwa akitoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika sekta ya afya kwa nchi nzima pamoja na utoaji wa fedha kwa ajili ya ununuaji wa vifaa tiba; kwa Wilaya ya Kongwa kwa mfano, kuanzia mwaka 2015 hadi leo, Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya, katika Vituo vya Afya vya Mlali, Ugogoni, Mkoka na Mbande. Aidha, Serikali imetoa takribani shilingi milioni 700 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa Vituo vya Afya Mlali na Ugogoni.
Dkt. Serera ametaka majengo hayo ya Kituo cha Afya Ugogoni yalindwe na kutoa wito kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwanza kuiunga mkono serikali yetu katika uchaguzi ujao ili iendelee kuboresha afya za wananchi, pili kupata huduma za afya kwenye vituo vya huduma za afya ambavyo vimejengwa na serikali kwa gharama kubwa ikihusisha Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati, hivyo, watumie fursa ya vifaa vya kisasa vilivyowekwa katika Kituo cha Afya Ugogoni.
Mwishowe, Dkt. Serera amewahasa wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF ili kupunguza gharama za matibabu pamoja na kulinda na kutunza amani ya nchi iliyopo. Na kumalizia kwamba yeye amekuja kuunganisha pale tulipoanzia.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mwl. Abdi amewahasa vijana; “Vijana msilale ninyi ndiyo wenye dhamana kubwa ya kuongoza nchi hii, mkirudi nyuma kwa sababu ninyi ndio mtakuwa mababa wa kesho, wazee wa kesho, akina yaya umri unaenda, sisi tuanitwa watu wa danger zone, kwani watu wa danger zone saa yeyote waweza kurusha miguu juu, kwaheri unaenda zako, kwa hiyo vijana mchangamke” hayo amesema.
Aidha, amesema kuwa Mkuu wa Wilaya aliyekuja anamtambua kuwa ni kijana chapa kazi, hodari, yeye amekulia kwenye Chama, amelelewa vizuri na hakika kutakuwa na mabadiliko makubwa sana yatatokea katika Wilaya ya Kongwa.
Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary A. Nkullo naye amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa maono aliyokuwa nayo kwenye sekta ya afya na amefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya.
Aidha, Dkt. Omary A. Nkullo ameeleza kwamba kwa Wilaya ya Kongwa, mapinduzi hayo makubwa sekta ya afya leo hii tunayashuhudia katika Kituo cha Afya Ugogoni; lakini tumejenga Kituo cha Afya Mlali, tumejenga na tunaendelea kujenga Hospitali ya Wilaya, tunaongeza majengo pale. Lakini tunaendelea kujenga kituo cha Afya Mbande, ambacho ni kituo kipya kabisa na kituo cha afya mkoka, vyote hivyo ujenzi unaendelea mengine yamekamilika. Kituo cha Afya Ugogoni kilipokea fedha shilingi milioni mia nne kiasi ambacho kimetumika kujenga majengo matano, likiwemo hilo la upasuaji, mama na mtoto, maabara, nyuma ya mtumishi na nyumba ya kihifadhia maiti.
Pia, Dkt. Omary A. Nkullo ameipongeza kamati ya ujenzi iliyoshiriki katika ujenzi wa Kituo hicho kwa umakini na uaminifu waliyouonesha wakati wa ujenzi.
Nkinde Moses
Afisa TEHAMA
Halmashauri ya Wilaya
Kongwa
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.