Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa inaendelea kujikita katika uboreshaji wa mkakati wa utoaji lishe katika shule za msingi na sekondari ilikuchochea matokeo mazuri ya wanafunzi Pamoja na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni.
Hayo yameelezwa na Afisa elimu msingi Wilaya ya Kongwa bi Margreth Temu alipokuwa akitoa taarifa ya lishe shuleni ambapo amesema kuwa asilimia 100 ya shule za msingi Wilayani Kongwa, wanafunzi wake wanakula chakula shuleni.
Aidha Mwl. Magreth Temu amefafanua kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji hali inayopelekea kukwamisha upandaji wa miti ya matunda ambapo upandwaji miti ya matunda kwa wingi ungeongeza tija katika swala la lishe shuleni kwani wanafunzi wangepata matunda katika chakula wanachopata shuleni ili kuongeza virutubisho katika ukuaji wao. Bi Magreth ameongeza kuwa kila shule imeunda klabu ya mazingira ili kusimamia suala la usafi wa mazingira na upandaji miti kwa wingi Pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Kongwa Bwana Msafiri Mkunda ameeleza kuwa katika robo ya pili ya Oktoba/Desemba 2024, Idara imeweza kuandaa mashamba darasa kwa shule za sekondari na msingi 172 na kusambaza tani 7 za mtama utakaopandwa katika mashamba hayo ili kusudi mavuno yatumike kama chakula shuleni. Ameongeza kuwa uamuzi wa kuchagua mbegu za mtama ni wa kisayansi kwani mbegu hizo zinaweza kukabiliana na hali ya ukame hivyo kusaidia kuwepo kwa mavuno baada ya msimu wa kulima kuisha.
Nae Afisa lishe Wilaya ya Kongwa Bi. Maria Haule amesema wamefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokula shuleni kutoka 83% kwa kipindi cha July-Sept 2024 hadi 90.2% kwa kipindi cha Oktoba-Disemba 2024 na dhumuni ni kuhakikisha kuwa wanafunzi asilimia mia moja wanapata chakula Shuleni kama jinsi malengo yanavyoelekeza.
Nae mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt Omary Nkullo amesema taarifa ya lishe itolewe mapema na mara kwa mara ili kusaidia utekelezaji na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika kutekeleza mkakati wa kuhakikisha wanafunzi asilimia mia moja wanapata chakula shuleni.
Akifunga kikao hicho mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka amewataka Watendaji wa Vijiji na kata kufanya kazi kwa ufanisi ili matokeo ya kazi zao yaonekane katika jamii "uongozi ni matokeo tusipike taarifa" na suala la chakula shuleni ni mkataba wa lazima.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.