Na Stephen Jackson na Nkinde , Kongwa.
Halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma inatekeleza mradi wa mazingira ili kuiwezesha kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhe. Dkt. Samwel G. Mafwenga wakati alipokuwa akihutubia katika Mkutano wa uzinduzi wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za wakulima na wafugaji wilayani Kongwa tarehe 12, Oktoba 2021 katika ukumbi wa chuo cha VETA wilayani Kongwa.
Katika hotuba yake pia alieleza kuwa mwishoni mwa Mwaka 2017 taasisi anayoisimami (NEMC) ilipata ithibati ya kuwa wakala wa taifa wa mfuko wa kimataifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Kufuatia hatua hiyo ya kuthibitishwa na kuwa mwangalizi wa miradi ya mazingira, Shirika la Foundation for Energy Climate and Environment (FECE), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kongwa waliandika andiko la mradi lililokubalika kimataifa na kuwa miongoni mwa maandiko manne (4) yaliyoidhinishwa kati ya maandiko mia moja na sita (106) yaliyowasilishwa.
Aidha Dkt. Mafwenga ameelezea kufarijika na kazi aliyoifanya Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbunge wa jimbo la Kongwa Mhe. Job Yustino Ndugai kwa jitihada zake zilizopelekea kufanikiwa kwa mradi huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni moja na laki mbili sawa na Tzs. Bilioni 2.7.
Kwa upande wake Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai (Mb) ameshukuru sana kutolewa kwa Fedha hizo kwani zitasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Ndugai Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa vijiji ambavyo mradi huo unatekelezwa, kuupokea kwa mikono miwili kwa kuwa mradi huo ni mzuri kwani utahusisha usambazaji wa maji, na pia miradi ya kilimo cha mazao mbalimbali kama vile mtama, ufuta viazi vitamu n.k na pia utawezesha utoaji wa mafunzo mbalimbali.
Akitolea ufafanuzi kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Foundation for energy climate and Environment (FECE) Dkt. Dominico Klemo ameeleza kuwa mradi huu wa miaka mitatu utatekelezwa na shirika hilo kwa kushirikiana na wilaya ya Kongwa chini ya uangalizi wa NEMC lengo likiwa ni kuzinufaisha Kata mbili za Ugogoni na Mtanana.
Mradi huu wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi unalenga kusaidia upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wakazi wa kata husika, Kuwezesha shughuli za wananchi kuwa endelevu, kutunza mazingira ili yaweze kuwalinda wananchi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kujenga uwezo wa taasisi na maafisa katika wilaya ya Kongwa juu ya namna bora ya kukabiliana na Majanga yanayoweza kujitokeza.
Akihitimisha Mkutano huo wa uzinduzi wa mradi, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emanuel amewataka wasimamizi wa mradi huo kuwa wazalendo ili malengo ya mradi huo yaweze kutimia.
Mradi huu umezinduliwa rasmi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai mbele ya Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emanuel na viongozi mbalimbali na wadau wa mazingira wilayani Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.