Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC) imewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kusimamia vizuri ujenzi wa miradi kupitia Fedha zinazotolewa na Serikali.
Akiwasilisha Taarifa ya ujenzi wa wodi tatu za Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya, Dkt. Thomas Ndalio Samweli, Mganga Mkuu Wilaya alieleza kuwa, kiasi cha shilingi 750,000,000.00 kilipokelewa mnamo Mwezi Disemba 2022, kwa ajili ya ujenzi wa wodi, na jumla ya Shilingi 623,808,220.00 zimetumika kujenga wodi hizo ambazo ni wodi ya wanaume, wanawake na watoto na ujenzi umekamilika kwa asilimia 98% na Fedha zilizosalia zimetumika kuboresha miundombinu mingine ikiwemo jengo la wazazi.
Akihutubia katika ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati Mhe. Stanslaus Mabula (Mb) aliwapongeza viongozi Wilayani Kongwa kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha na hivyo kutimiza malengo ya Serikali, huku Dhamira ya kamati hiyo ikiwa ni kuona thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa.
Akihutubia wananchi wa Kata ya Chiwe katika Shule ya Msingi Moleti iliyojengwa Kwa zaidi ya Milioni 300 kupitia mradi wa BOOST, amewataka wananchi kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali ili iweze kuleta manufaa Kwa jamii husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alisema kupitia mradi wa BOOST Mkoa wa Dodoma ulipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10 na Milioni 600 zilizotumika kujenga Shule mpya 16, madarasa 103, vyoo na miundombinu mbalimbali ambayo imechangia mabadiliko makubwa katika sekta ya Elimu.
Aidha Mhe. Senyamule ametumia fursa hivyo kuipongeza kamati ya Bunge Kwa mchango wake mahsusi katika kufanikisha miradi.
Naye Dkt. Festo Dugange Naibu waziri Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa ameishukuru kamati hiyo Kwa kutembelea na kukagua miradi, huku akiungana na wananchi kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kutoa Fedha Shilingi Milioni 318 Kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Moleti kupitia mradi wa BOOST.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Bwn. Fortunatus Mabula aliwasilisha Taarifa fupi ya utekelezaji miradi husika.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.