Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepongezwa kwa kupokea hati Safi ya uendeshaji wa shughuli zake kwa kipindi cha miaka mitano ya 2020-2025
Akitoa pongezi hizo katika mkutano wa Baraza la Madiwani la kujadili taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali, Afisa kutoka Ofisi ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali Bw. Karim Mwinyimbegu amesema kuwa kupata hati inayoridhisha ni pamoja na utekelezaji wa hoja zilizokuwepo katika kipindi cha miaka mitano.
Pamoja na kushukuru kwa ushirikiano mzuri wa viongozi uliopo lakini pia Bw. Mwinyimbegu amesema kuwa kutokana na hoja hizo anashauri Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ifanyie kazi, ikague hatua kwa hatua fedha zilizolipwa kimakosa ili ziweze kurejeshwa, ifatilie dawa na vifaa tiba katika bohari ya dawa ili kupata dawa na vifaa tiba vilivyonunuliwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Akifafanua namna hati safi ilivyopatikana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt Omary Nkullo amesema kuwa hati safi zimepatikana kutokana na usimamizi mzuri wa mifumo ya udhibiti wa ndani pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo.
Aidha Dkt. Nkullo ameeleza changamoto zilizopelekea kuchelewa kujibu baadhi ya hoja kuwa ni pamoja na hoja zilizo nje ya uwezo wa Halmashauri kama upungufu wa wataalam katika fani mbalimbali ambapo Halmashauri imeendelea kuandika barua mara kwa mara kuomba watumishi na kuongeza kuwa Halmashauri imejipanga kuzimaliza hoja zote ambazo hazijakamilika.
Akisoma taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka, ameeleza kuwa kutokana na taarifa ya mdhibiti wa hesabu za Serikali, anasisitiza kamati ya fedha ije na ajenda ya kudumu kujibu hoja za Mdhibiti, pamoja na hayo pia amesisitiza ujenzi wa jengo la utawala kukamilika kufikia Mwaka wa fedha 2025/26.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.