Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthon Mtaka, amewashauri viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kubuni Miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo itaiwezesha Wilaya kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato badala ya kutegemea ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye miradi binafsi ya wananchi.
Kiongozi huyo wa Mkoa, ametilia mkazo uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo ikiwemo alizeti kama sehemu ya kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kongwa.
Mheshimiwa Mtaka aliyasema hayo wakati alipokuwa akihutubia Mamia ya Wananchi waliojitokeza katika Kuadhimisha kumbukumbu ya miaka Sitini (60) ya Uhuru wa Tanganyika akiwa ni mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo.
Katika hotuba yake alisisitiza matumizi sahihi ya Mawazo ya Wataalamu katika vikao mbalimbali vya Halmashauri pamoja na matumizi ya Taaluma na ubunifu kwenye utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Katika Maadhimisho hayo, jumla ya pikipiki 12 zenye thamani ya TZS. Milioni Thelathini (30,000,000/=) zimetolewa kwa vijana wa Bodaboda kama sehemu ya mikopo inayotokana na 10% ya mapato ambayo hutolewa na Halmashauri kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii.
Wakati huohuo hundi yenye thamani ya Tshs. Milioni miamoja tisini na tatu, Mia sita Thelathini na Mbili Elfu na Miatano (193,632,500/=), Kutoka Benki ya ‘’NMB’’ ilikabidhiwa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu.
Akitoa shukrani mara baada ya Hotuba hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Emmanuel, ameahidi kushirikiana na viongozi wa Halmashauri kutekeleza ushauri uliotolewa.
Maadhimisho hayo Kimkoa yalifanyika Disemba 8, 2021 Wilayani Kongwa, katika eneo la kituo cha mabasi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali (kimkoa) huku yakipambwa na burudani mbalimbali kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa wilayani Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.