Jumla ya miradi minne (4) yenye thamani ya Tsh. 1,744,901,951/= imepitiwa na Mwenge wa Uhuru ambapo Halmashauri ya Wilaya imechangia Tsh. 68,992,500/=, Wahisani Tsh. 371,737,200/=,
Serikali Kuu Tsh. 1,225,552,251/=, Sekta binafsi 70,000,000/= na Wananchi Tsh. 8,620,000/= .
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Wilayani Kongwa umefanya shughuli zifuatazo; Kuweka jiwe la Msingi Ujenzi wa miundombinu katika kituo cha Afya Mlali; Kuzindua Ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Sekondari Laikala; Kufungua Mradi wa Maji katika Kijiji cha Machenje; Kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Kituo cha Kongano la Biashara ya Kuku wa Asili.
Mradi wa Kituo cha Afya Mlali:
Imeelezwa kwamba mradi hadi kufikia siku ya kupitiwa na Mwenge wa Uhuru umekamilika kwa asilimia 95 ambapo jumla ya majengo matano (5) yamejengwa. Majengo hayo ni Nyumba ya Mtumishi, Jengo la kuhifadhi Maiti, Jengo la Maabara, Jengo la Wodi ya Akina Mama na Jengo la huduma ya Upasuaji. Mradi huu umegharimu kiasi cha Tsh.408,216,000/= kati ya fedha hizi; Tsh.400,000,000/= zimetolewa na Serikali, Tsh.4,596,000/= zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya na zilitumika kwa ajili ya shughuli mbali mbali za usimamizi wa ujenzi wa Majengo. Wananchi wamechangia Tsh.3,620,000/= kwa kutoa nguvu zao
kwa kufanya usafi katika eneo la kituo pamoja na kufanya usimamizi kupitia Kamati za Ujenzi, Manunuzi na Mapokezi. Mradi huu utaboresha mazingira ya kutolea huduma za Afya na pia utasaidia kuboresha makazi ya watumishi. Aidha mradi huu utasaidia kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi.
Mradi wa Ujenzi wa Madarasa Shule ya Sekondari Laikala:
Mradi umetekelezwa na Halmashauri kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (P4R). Lengo la Mradi huu ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Elimu bila malipo. Miundombinu hii inatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza katika mazingira rafiki na wezeshi. Mradi huu umekamilika na umegharimu jumla ya shilingi 86,600,000, kati ya fedha hizi Tsh. 80,000,000/= zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 4 na viti/meza 160 na Tsh. 6,600,000/= zimetumika kujenga matundu 6 ya vyoo.
Mradi wa Maji katika Kijiji cha Machenje:
Mradi ulianza tarehe 07/07/2017 na umekamilika tarehe 30/06/2018, Mradi umejengwa na Mkandarasi NOLC ENGINNERING CO. LTD ukiwa na lengo kuu la mradi ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Kijiji cha Machenje kutoka 21% Mwaka 2015/2016 hadi 100% Mwaka 2017/2018. Gharama za Mradi huu ni Tsh. 743,952,251/= kwa mchanganuo ufuatao; Mchango wa Serikali Kuu na Wahisani wa Maendeleo 738,952,251/=; Wananchi 5,000,000/=.
Mradi wa Kongano la Biashara ya kuku wa Asili Wilaya ya Kongwa:
Wazo la mradi lilitokea katika Idara ya Mifugo na Uvuvi baada ya kuona changamoto katika masoko ya kuku wa asili. Mradi huu upo katika mfumo wa kongano (Cluster) ambapo wadau mbalimbali wanahusika katika utekelezaji wa mradi. Wadau wanaohusika katika kutekeleza mradi huu ni pamoja na wafugaji wa kuku, wauzaji wa pembejeo zinazotumika katika ufugaji wa kuku kama vile vyakula, vyombo vya chakula na maji, wauza madawa na wauza vifaranga. Mradi utaanza kutekelezwa katika kata tano ambazo ni Kongwa, Sejeli, Mkoka, Mtanana na Kibaigwa. Wafugaji kutoka katika kata zingine wataongezwa kadiri utekelezaji utakavyokuwa ukiendelea.
Lengo la mradi ni kuboresha kipato cha Mwananchi mmoja mmoja na Halmashauri kwa ujumla kwa kuwaunganisha wafugaji wa kuku wa asili kwa pamoja ili kupata soko la kuku na mazao yake.
Mradi hadi utakapokamilika unatarajiwa kugharimu Tsh. 506,133,700/=, kati ya hizo; Tsh 70,000,000/= tunatarajia kukopa benki, Halmashauri itachangia Tsh 64,396,500/= na Wahisani Serikali ya Denmark kupitia mradi wa Local Investment Climate (LIC) wanatarajia kuchangia Tsh. 371,737,200/=. Hadi sasa jumla ya Tsh. 243,362,500/= zimeshapatikana kutoka LIC na jumla ya Tsh. 168,136,999/= zimeshatumika.
Aidha, katika miradinyote iliyopitiwa na Mbio hizi za Mwenge wa Uhuru hakuna mradi uliotolewa kasoro au dosari na kukatliwa na Kiongozi Mkuu wa Mbio hizo Mhe Harles Francis Kabeho.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 umebeba Ujumbe unaosema; Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza sasa kwa Maendeleo ya Taifa letu”. Sanjari na ujumbe huu ni, Tuwasikilize na kuwashauri Watoto ili wasitumie Dawa za kulevya, mapambano dhidi ya Rushwa “Kataa Rushwa- Jenga Tanzania” mapambano dhidi ya Ukimwi “Mwananchi Jitambue pima Afya yako sasa” na mapambano dhidi ya Malaria “Shiriki kutokomeza Malaria”.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.