Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ameongoza zoezi la upandaji miti ikiwa ni moja ya shughuli za kijamii alizoshiriki kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara inapotimiza miaka 63 ya Uhuru wake.
Mhe. Mayeka ameongoza zoezi hilo katika viunga vya chuo cha ufundi stadi Veta Kongwa ambapo amesema kuwa kuelekea sherehe za miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara, wananchi wote hususa ni vijana waendelee kuyaenzi mafanikio na jitihada mahsusi zilizopelekea kufikia miaka hiyo huku akisisitiza watanzania wote kuilinda Tanzania kwa wivu mkubwa kwani hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania na kuongeza kuwa hapa ndiyo nyumbani kwetu.
Aidha Mhe. Mayeka amehimiza wananchi kuzingatia kampeni ya "Mti wangu birthday yangu" na kuwataka wananchi kuwa na desturi ya kupanda mti walau mmoja kila mwaka wanaposherehekea miaka kadhaa ya kuzaliwa kwao ili kuweze kuwa na mazingira mazuri na uboreshwaji wa hali ya hewa.
Vilevile Mhe. Mayeka amewapongeza wananchi wa maeneo mbalimbali wilayani Kongwa ambao wamefanya usafi wa mazingira na kupanda miti katika maeneo yao lengo likiwa ni kuweka kumbukumbu nzuri ya kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka huu 2024.
Mhe. Mayeka pia ametumia wasaa huo kutoa rai kwa wananchi wa mji mdogo wa Kongwa kuacha kupanda mazao marefu kama mahindi, mtama na alizeti katika maeneo ya viunga vya mji na kuwahimiza viongozi waendelee kutoa elimu kwa wananchi juu ya sifa na sheria za mji zinavyoelekeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upandaji miti na ameomba zoezi hilo liwe endelevu ili katika Wilaya ya Kongwa kupatikane miti ya kutosha kuweza kuhimili mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuleta muonekano mzuri wa mazingira.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.