MAADHIMISHO YA 33 YA WIKI YA UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA YAFANYIKA KONGWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Imeelezwa kuwa suala la unyonyeshaji ni msingi wa ukuaji bora wa mtoto na kwamba lishe duni huleta ulemavu na unyonyeshaji duni huathiri ukuaji wa mtoto kiakili, kimwili na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa na Bi Margreth Temu Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa alipomwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika maadhimisho ya 33 ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama yaliyofanyika katika Kijiji cha Ibwaga Kata ya Ugogoni Wilayani Kongwa.
Bi. Margreth Temu Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kongwa akiongea na wananchi katika maadhimisho hayo
Aidha Bi. Temu amefaafnua kuwa zipo sababu za akina mama kushindwa kunyonyesha zikiwemo kazi nyingi shughuli za utafutaji na mila potofu lakini ni jukumu la jamii yote kuweka mazingira mazuri ya unyonyeshaji kuwapatia lishe bora akina mama wanaonyonyesha ikiwemo kuwapatia mlo kamili.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Thomas Mchomvu amewataka akina mama kuzingatia kanuni za afya ili waepukane na utapiamlo mkali na madhara yake kama vifo kwa Watoto na kuzingatia maziwa salama ya mama kwa watoto na sio maziwa ya Wanyama.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Thomas Mchomvu akiongea na wananchi katika maadhimisho hayo
Kwa upande wake Bi. Mary Haule Afisa lishe Wilaya amesema kwa kipindi cha mwaka 2024 watoto waliozaliwa sawa na 99% walinyonya maziwa ya mama pekee na kati yao 5% sawa na watoto 1,720 hawakunyonya maziwa hayo pekee katika kipindi cha miezi sita na kati yao asilimia 31 ya Watoto hao wamedumaa.
Baadhi ya akina mama wakipatiwa huduma za afya katika maadhimisho hayo
Akiongea kwa niaba ya akina mama wenzie Bi. Roda Majuto mkazi wa Kijiji cha Ibwaga amesema maadhimisho yamewawezesha kujifunza kuwa unyonyeshaji mzuri ni miezi sita bila kumpatia mtoto chakula chochote mbadala na baada ya hapo apate lishe bora.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.