"Kila mmoja wetu akitimiza majukumu yake kwa kufuata Sheria na taratibu, Serikali haitapoteza fedha kutokana na vikundi kushindwa kulipa mikopo."
Hayo yameelezwa Oktoba 29 2024 na Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Kongwa Bw Cosmas Shauri wakati akitoa semina kwa maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kongwa kuhusu kupambana na kuzuia mianya ya Rushwa katika mchakato wa utoaji wa mikopo 10% kwa vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu.
Bwana Shauri amesema utoaji mikopo wa awali haukuwa mzuri sana na kupelekea hadi sasa vikundi vingi bado vinadaiwa hivyo taasisi imeona ni vema kutoa elimu hii ili kusaidia maafisa hao kutambua na kusimamia vema majukumu yao ili kufanikisha kupata vikundi vyenye sifa ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati na kuiepushia serikali hasara.
Kwa upande wake Bw Peter Makwaya kutoka Kata ya Hogoro amesema semina hiyo itamsaidia katika kazi yake ya kutoa mikopo, kutambua kuwa kuzuia na kupambana na rushwa si kazi ya TAKUKURU bali ni jukumu la kila mwanajamii, pia wananchi wanatakiwa wafahamu kuwa kupata mikopo ni haki yao bila kutoa fedha wala zawadi yoyote kwa maafisa Maendeleo ya Jamii au kiongozi yeyote ili wapate mikopo hiyo.
Nae Bi Betha Mwanitu amesema amejifunza mambo mengi kuhusiana na rushwa katika kazi yake ya kushughulikia vikundi vinavyohitaji mikopo kwamba katika majukumu ya kila siku mwananchi anaweza kutengeneza mazingira ya kutoa rushwa Kwa kukupa zawadi ili umfanyie jambo fulani, au mwananchi anaweza kumfata kiongozi nje ya muda wa kazi ili kuomba huduma fulani kwa upendeleo ambapo anaweza kutengeneza mazingira ya rushwa.
Bi Betha ameweka wazi kuwa semina hiyo ni muhimu sana kwao na pia maafisa Maendeleo ya Jamii wataepukana na mazingira yote yanayoweza kujitokeza yanayoaashiria utoaji au upokeaji wa rushwa kwani ni wajibu wao kama viongozi kuwahudumia wananchi wote lakini ni lazima wawe makini na kufanya kazi kwa uadilifu bila kumpendelea mtu yeyote.
Semina hiyo iliyofanywa na ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Kongwa ni mwendelezo wa semina nyingi zinazofanywa kwa makundi mbalimbali yakiwemo kama maafisa wa polisi, viongozi wa dini na Sasa maafisa Maendeleo ya Jamii lengo likiwa ni kudhibiti mianya ya Rushwa katika jamii hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.