Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai ameyataka Mabaraza ya Migogoro Wilayani Kongwa kutoa haki kwa Wananchi ili kudumisha amani katika maeneo yao.
Mhe. Ndugai amesema hayo Mei 23, 2024 katika kikao cha Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango wakati wa kujadili agenda ya yatokanayo na kikao kilichopita, ambapo iliazimiwa Mabaraza yote yaliyokosa sifa kwa kumaliza muda wake yahuishwe.
Mhe. Ndugai ametoa wito kwa wajumbe wa Mabaraza hayo kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki wakati wa maamuzi yao, badala ya kuwa kikwazo cha upatikanaji wa haki.
Kuhusu ustawi wa watumishi, Mhe. Ndugai ameshauri watumishi kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa SACCOS ili kupunguza changamoto za kiuchumi baina yao.
Akifafanua hoja hiyo, Mkuu wa Kitengo cha huduma za Kisheria Wakili Hella Mlimanazi alisema, mchakato huo unaendelea chini ya Kamati za maendeleo za Kata, ambapo jumla ya Mabaraza 13 yaliyomaliza muda wake yanatarajiwa kuhuishwa chini ya maelekezo ya Halmashauri katika kipindi cha siku kumi na nne (14) kuanzia Mei 21, 2024.
Kwa mujibu wa Maelekezo, Mabaraza hayo hushugulikia migogoro ya Ardhi, familia na jinai ndogo ndogo kwa lengo la kukuza dhana ya usuluhishi baina ya Wananchi.
Akijibu hoja ya Mkaguzi wa ndani bwana Jacob Mgusi iliyojikita kwenye uhafifu wa marejesho ya mikopo ya Asilimia 10% iliyotolewa kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Jinsia wanawake na Makundi Maalumu, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, wanawake na Makundi Maalumu Bi. Paskalina Duwe amesema takribani shilingi milioni 482 zinadaiwa kutoka kwa vikundi, hivyo ameiomba Menejimenti kutatua changamoto ya usafiri ili kuongeza kasi ya ufuatiliaji.
Akihitimisha kikao hicho Mhe. White Zuberi Mwanzalila Mwenyekiti wa Halmashauri, amewataka Wakuu wa Divisheni na Vitengo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali, ikiwa ni pamoja na fedha za ujenzi wa Jengo jipya la Halmashauri.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.