Kuelekea katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Halmashauri ya wilaya ya Kongwa imekuja na siku maalumu za wananchi kukutana katika viwanja mbalimbali vya michezo ili kushiriki katika michezo mbalimbali kwa dhumuni la kutoa ujumbe wa kuhamasisha ushiriki wao katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mashindano ya kuvuta Kamba, kukimbia kwenye magunia, kufukuza kuku na mingine mingi imekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi waliohudhuria mabonanza hayo yaliyofanyika katika Kata mbalimbali za wilaya ya kongwa.
timu ya bodaboda ya wasafi katika picha ya pamoja kwenye siku ya bonanza Kongwa.
Akiongea na wananchi waliojitokeza tarehe 16 Septemba katika ufunguzi wa bonanza lililofanyika katika Kata ya Kongwa kabla ya kutoa zawadi kwa washindi, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi wao katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na kuwaeleza kuwa ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka, basi inabidi wakajiandikishe pindi zoezi litakapoanza kwani kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ni msingi wa uchaguzi bora.
Aidha mhe. Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wananchi waliohamia maeneo ya Kata ya Kongwa kuandikisha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura, na wananchi ambao ni wakazi wa Kata ya Kongwa kuhakiki taarifa zao katika daftari hilo ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaoamini watawaletea maendeleo katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika siku za usoni.
Pichani ni Mhe Mayeka Simon Mayeka akikabidhi zawadi kwa mshindi wa mashindano ya mpira.
Siku ya alhamisi ya tarehe 19 Septemba Katika kata ya Mlali, ushindani mkubwa wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu ya Bafana bafana na timu ya New-star ulikuwa na msisimko mkubwa ambapo Bafana bafana walipata ushindi mwembamba wa goli moja ambalo liliwafanya waibuke kidedea na kupatiwa zawadi na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa dkt. Omary Nkullo. Akiongea wakati akitoa zawadi dkt Nkullo alihamasisha umati wa watu uliojitokeza uwanjani kushiriki kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Mkurugenzi mtendaji pia alisisitiza vijana ambao wana umri wa miaka kumi na saba wajitokeze kujiandikisha kwani uchaguzi mkuu wa mwaka ujao watakuwa wana umri wa kupiga kura.
Pichani ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa akikabidhi zawadi kwa timu ya Bafanabafana.
Kata ya Hogoro ndiyo Kata iliyotia fora katika mahudhurio katika mabonanza yote yaliyofanyika katika wilaya ya Kongwa. Umati wa wananchi wa Kata ya Hogoro ulipata wasaa wa kushuhudia burudani ya mechi ya mpira wa miguu kwa wanawake ambapo ushindani mkubwa baina ya timu zilizoshiriki ulikuwa kivutio kikubwa sana. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa akitoa zawadi, alifikisha ujumbe kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na wananchi walionyesha kuelewa ujumbe huo muhimu.
Umati wa watu waliojitokeza kutazama michezo mbalimbali katika bonanza.
Kilele cha mabonanza haya yaliyobeba msisimko mkubwa wa kukusanya wananchi waliojitokeza kwa wingi kushangilia timu zao kilifanyika katika Kata na Kibaigwa na kisha Kata ya Mkoka ambapo wananchi walipata wasaa wa kusikiliza viongozi wao ikiwemo madiwani wa Kata hizo wakitoa wito juu ya ushiriki wao katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Itoshe kusema kuwa mabonanza haya yamekuwa chachu ya kukusanya wananchi na katika kila bonanza imetolewa elimu juu ya umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Kazi inabaki kwa wananchi kutimiza wajibu huo na kuitikia wito huo ili kuweza kutimiza haki yao ya kikatika ya kupiga kura pindi chaguzi za viongozi zitakapoanza.
Katika wilaya ya Kongwa, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura limemalizika na hivi sasa zoezi linalofuata ni uandikishaji wa wapiga kura ambapo zoezi hilo ni maalum kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaoanza tarehe 27 mwezi wa kumi na moja mwaka huu. ni muhimu kwa wananci kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka wawaletee maendeleo
Imeandaliwa na;
Mbonea E. Masha
Afisa Habari wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.