MAGEREZA KONGWA YAJIVUNIA MIAKA 64 YA UREKEBU KWA WAFUNGWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Maadhimisho ya miaka 64 ya Jeshi la Magereza Tanzania Bara, Kongwa wajivunia kuwa na Gereza Kongwe la tangu enzi za mkoloni mwaka 1949 lenye historia kubwa kutokana na mabadiliko makubwa ya kubadilisha tabia za wafungwa katika jamii.
Akiongea katika maadhimisho hayo SSP Tekla Erasto Ngilangwa Mkuu wa Gereza la Kongwa amesema Jeshi la magereza katika kuhitimisha maadhimisho hayo yaliyoanza agosti 23 yenye kaulimbiu "Ushirikiano wa Jeshi la Magereza na Jamii kwa Urekebishaji Wenye Tija" inataka jamii iweze kuona mchango wa Jeshi hilo katika urekebu wa tabia.
Akiongea wakati wa kukabidhi misaada katika kituo cha watoto wenye ulemavu Mlali SSP Ngilangwa ameeleza kuwa Jeshi la Magereza linatambua mazingira magumu wanayopitia walezi katika kuwalea na kuwahudumia watoto hao na kwamba kwa kufanya hivyo wanaisaidia sana Serikali.
Kwa upande wake Padri Gaudence Shayo Mkurugenzi wa kituo cha watoto wenye ulemavu Mlali ameshukuru Jeshi la Magereza kwa huduma ya misaada waliyoitoa na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kuhudumia jamii nyingine zenye uhitaji.
Jeshi la Magereza Kongwa, pia limetoa msaaada katika kituo cha Watoto wenye ulemavu wa wa akili na uziwi kilichopo shule ya msingi kongwa ambapo Mwalimu mkuu msaidizi wa kituo hicho Mwl. Akulu Mongele ameelezea furaha yake kwa kutembelewa na jeshi hilo na kupatiwa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwani huo ni upendo wa dhati.
Katika maadhimisho hayo Jeshi la Magereza Wilaya ya Kongwa limefanya usafi katika Vituo vya kutolea huduma za afya, Uchangiaji Damu na kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji, walemavu na watoto yatima na kuwafikia watu wote wenye uhitaji.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.