Na Stephen Jackson, Kongwa
Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, wamehudhuria Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Viti maalumu kata ya Matongoro, Marehemu Sarah Elia Lujeli ambaye amefariki dunia tarehe 2 Agosti 2021 katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Akizungumza na waombolezaji, Mhe. Mwema amewasisitiza waombolezaji kutambua thamani ya uhai wao na kuujali, hivyo wanao wajibu wa kuchukua Tahadhali dhidi ya ugonjwa hatari wa ‘’corona’’ na ameahidi kupata chanjo ya ugonjwa huo ambayo Kiwilaya ilipangwa kuzinduliwa tarehe 5 Agost 2021.
Kufuatia msiba huo, Salamu mbalimbali za rambirambi kutoka kwa viongozi wa Chama Tawala CCM, Halmashauri ya Kongwa na Makundi mbalimbali ya Kijamii zimetolewa.
Akiwasilisha salamu hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Afisa Tawala Ndugu Geofrey Mville alisema, Marehemu Sarah Elia Lujeli alizaliwa Tarehe 30 Desemba 1966 katika Kijiji cha Matongoro na alijiunga na duru za kisiasa tangu mwaka 1994 na kufanikiwa kushika wadhifa wa Diwani viti Maalumu pamoja na nyadhifa nyingine kwa nyakati tofauti hadi alipofikwa na umauti.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa White Zuberi Mwanzalila pamoja na kutoa salamu za pole kwa waombolezaji wote pia amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Lupa Kutoka Chunya Mbeya, Chief Masache Njelu Kasaka kwa jitihada za kuusafirisha mwili wa Marehemu Sarah kutoka mkoani Mbeya hadi kufikishwa nyumbani kwake Matongoro.
Kuhusu ugonjwa wa Covid 19 Mhe. White Zuberi Mwanzalila amewataka wananchi kuendelea kuchukua Tahadhari kwa kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono pia kupata chanjo ambayo imeanza kutolewa. "Na bahati nzuri zimeshaletwa chanjo. Chanjo ziko, tutakuwa na vituo vyetu vya Afya vitatoa huduma ya chanjo kwa yule anayetaka, na naamini baada ya muda mfupi, kila mmoja atachanja" Amesema White Zuberi Mwanzalila.
Akizungumza Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mbunge wa Jimbo la Lupa Chief Kasaka, amewataka wananchi kudumisha mazuri yote aliyoyafanya Marehemu Sarah kipindi cha Uhai wake Kama ishara ya kumkumbuka.
Aidha viongozi wengine wa CCM waliopata fursa ya kutoa salamu zao za rambirambi ni pamoja na Mhe. Pili Mbanga Katibu CCM Mkoa, Ferister Bura Mbunge Mstaafu viti maalumu Mkoa, Marco Mbanga Katibu CCM Wilaya ya Kongwa, Henry Msunga, Katibu Mwenezi CCM mkoa, na Mariam Kret Katibu UWT Mkoa.
Ibada ya mazishi ya Marehemu Sarah Elia Lujeli imeongozwa na Canon Jackson Lwanda wa kanisa la Anglikana Parishi ya Mkoka, na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa CCM ngazi ya Mkoa, wilaya, kata na kijiji, Uongozi wa Halmashauri, Madiwani na wananchi
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.