Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Remidius Mwema Emmanuel ameendesha Kikao maalum na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi ndani ya Wilaya ya Kongwa chenye lengo kuu la kuweza kufahamiana wadau kwa wadau na Uongozi wa Wilaya ya Kongwa, kupata taarifa za kazi tangu utekelezaji wa mradi hadi wakati huu na Uongozi kuweza kutambua shughuli za wadau kwa kila eneo.
Mkutano huu umefanyika leo tarehe 30 Agosti, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ambapo jumla ya NGOs 16 zilishiriki na kutoa taarifa zao kuhusu shughuli mbalimbali wanazozifanya Wilayani Kongwa, changamoto wanazokumbana nazo, pamoja na kutoa maoni yao kwa uongozi wa Wilaya ya Kongwa kuhusu maendeleo ya Kongwa. Baadhi ya NGOs zilizoshiriki ni World Vision, TAYOA, TIST, KTP, TAFARMO, UFUNDIKO, Nurture Tanzania, ERGPAF, Compassion, BRAC, CCT Mwanamke Jasiri, LYVIA, CIS, Rafiki Dodoma na Wildaf.
Mhe Remedius ametoa maelekezo kwa NGOs zote kutoa taarifa zinazoendana na uhalisia na kutoa ushirikiano kwa Idara ya Maendeleo ya Jamii inayosimamia NGOs zote na idara zingine ambazo zinahusiana moja kwa moja na miradi inayofanyika ili miradi ifanyike katika maeneo yenye mahitaji zaidi.
Mhe Remidius pia, amezihakikishia NGOs zote kwamba, kila NGO inavyofanya kazi Wilayani Kongwa ataitembelea kuona shughuli zake katika maeneo husika na atatoa vyeti vya utambuzi kwa kila NGO kutambua mchango wake katika maendeleo ya Wilaya ya Kongwa.
“NGO yeyote inapopata changamoto katika maeneo inapofanyakazi isisite kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya yupo ili kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali”, amesema Mhe Remidius.
Mhe Remidius ameagiza NGOs zote ambazo hazikufika katika Kikao bila taarifa ziandikiwe barua kwani zinachafua NGOs zingine zinazofanya kazi vizuri katika Wilaya ya Kongwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuandaa fomati ya taarifa ambayo kila Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) itaitumia katika kuwasilisha taarifa zake Wilayani na NGOs hizo zikajipange na kuwasilisha taarifa rasmi kabla ya tarehe 10 Septemba 2021.
NGOs zilizoshiriki zimefurahi sana kwani hawakuwahi kukutana na wengi walikuwa hawafahamiani, hivyo, kikao hiki kimekuwa jukwaa zuri kwao kwa kuweza kufahamiana na kumuomba Mhe Mkuu wa Wilaya kufanya vikao hivi kila baada ya miezi 3, ambapo ombi lao limeridhiwa.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bibi Paskalina T. Duwe akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji Wilaya amesema vikao vya kukutana na NGOs ni vya kisheria na Idara yake imejipanga katika kuhakikisha vikao kama hiki vinafanyika kila baada ya miezi 3 na kuziomba NGOs kutoa ushirikiano kwa baadhi ya mambo yatakayo hitajika kutoka kwao kwa maandalizi ya vikao.
Mwisho, Mhe Remidius amezikaribisha NGOs zote kushiriki Kongamano la Maendeleo ya Wilaya ya Kongwa litakalofanyika tarehe 11 Septemba, 2021 katika Ukumbi wa VETA Kongwa ambapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa Mhe Job Ndugai, Viongozi wote wa Wilaya, Waheshimiwa Madiwani wa Kongwa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Kongwa watakuwepo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.