Na Stephen Jackson, Kongwa
Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika mstaafu wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai amewataka viongozi wanaoshughulikia maslahi ya walimu ikiwemo upandaji wa Madaraja kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu Ili kuharakisha upatikanaji wa haki za walimu.
Mhe. Ndugai, ameeleza hayo wakati alipokuwa akihutubia Mkutano mkuu wa nusu muhula wa chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kongwa, uliofanyika Jumamosi ya Tarehe 15 Oktoba, 2022 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kongwa.
Ameongeza kuwa kupitia dhamana aliyonayo kama mwakilishi wa wananchi, ataendelea kushirikiana na CWT katika kufanikisha upatikanaji wa haki za walimu hususani upandaji wa Madaraja.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kongwa Mwalimu Majuto Deus, pamoja na kumshukuru Mhe. Mbunge kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo, pia ameahidi kuwa CWT itahakikisha walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha wanafunzi na hatinaye kuinua ufaulu wa wanafunzi Wilayani Kongwa.
Kwa upande mwingine Mhe. Ndugai amewashauri wasimamizi wa shughuli za elimu kutoa fursa zinazopatikana kwa kuzingatia misingi ya usawa.
Kufuatia Ushauri huo, Afisa Elimu Msingi Bwn. Eugine Shirima, amekiri kuwepo kwa changamoto ya kujiridia rudia kwa wasimamizi wa mitihani hasa ya elimu ya msingi kutokana na sheria ya mitihani ambayo inawataka walimu wa shule za sekondari kusimamia mitihani ya shule za msingi, huku idadi yao Ikiwa ni ndogo ikilinganishwa na Idadi ya mikondo ya wanafunzi.
Naye Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Dodoma Mwalimu Samwel Malechela, amempongeza Mhe. Job Ndugai kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Maendeleo katika Jimbo la Kongwa hasa ujenzi wa miundombinu, zikiwemo barabara na Madarasa ya kisasa.
Nao wajumbe mbalimbali wa Mkutano wamewataka viongozi wa CWT kulinda na kusimamia vema mali za chama, na kufuatilia haki zao katika mifuko ya hifadhi ya jamii, bima ya Afya pamoja na taasisi za kiuchumi zinazohudumia walimu ikiwemo Benki ya Mwalimu.
Katika hatua nyingine Mkutano huo umepitisha azimio la kununua gari aina ya "Coaster" kwa ajili ya kutatua changamoto ya usafiri kwa wanachama kipindi wanapolazimika kusafiri kama chama kushiriki misiba na hafla mbalimbali huku chanzo Cha Fedha kikitajwa kuwa ni marejesho ya wanachama.
Mkutano huo umehusisha viongozi wa CWT ngazi ya Mkoa, Wilaya, uwakilishi mahala pa kazi pamoja na baadhi ya wadau wake ambao ni viongozi kutoka Halmashauri na Tume ya Utumishi wa walimu (TSC)
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.