Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai ameiasa jamii kuwa na utamaduni wa kusaidiana kiuchumi wenyewe kwa wenyewe badala ya kuacha jukumu hilo kwa wahisani.
Katika hotuba yake, Ndugai amesisitiza kuwa jamii ya watanzania inapaswa kuwa na utaratibu maalumu wa kuwasaidia watoto na vijana wanaotoka kwenye kaya maskini, sambamba na kuwalinda kimaadili.
Mhe. Ndugai amesema hayo wakati akizungumza na waumini wa kanisa Mt. Mathayo Anglikana - Kibaigwa, wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya huduma kwa mtoto na kijana ya shirika la "compassion" Aprili 13, 2024.
Akiwasilisha salamu za Mkurugenzi wa taifa wa Compassion International Tanzania (CIT) Mary Lema, Meneja wa shirika hilo Kanda ya kati Bi. AKinyi Kembi Migire, alisema Shirika linahudumia watoto wapatao 9033 katika vituo 51 vilivyopo katika Wilaya saba za Mkoa.
Alibainisha kuwa takribani jumla ya shilingi 60,000,000 hutumwa kwenye vituo (Klaster) saba Wilayani Kongwa kila mwezi sawa na shilingi 720,000,000 kwa mwaka mzima kwa ajili ya kuwaendeleza kielimu wanufaika wa shirika.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na makundi maalum Bi. Paskalina Duwe alisema, licha ya fursa ya kuwepo shirika la "Compassion" jamii inapaswa kutimiza wajibu wake kwa kuwalinda watoto kimaadlili ikiwemo watoto wa kiume.
Akiwakilisha Jeshi la Polisi Kongwa, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibaigwa ASP M. R. Msami alisema licha ya jeshi la polisi kuwa na dhamana ya kulinda Sheria za nchi, jamii nzima inapaswa kutimiza wajibu wake kikamilifu kwa kutofumbia macho vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa mujibu wa sheria.
Naye Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Kibaigwa Bi. Foska Mgovano ameitaka jamii ya kitanzania kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto kutimiza malengo yao kwa kuendeleza jitihada za wahisani wa shirika la Compassion.
Katika maadhimisho hayo, baadhi ya wanufaika wa malezi na msaada wa Compassion walitoa shuhuda mbalimbali za mafanikio.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.