Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Wadau wa Mazingira kutoka nchi mbalimbali, wamelipongeza Shirika lisilo la Kiserikali la Foundation for energy and climate change (FECE) kwa kufanikisha miradi ya mabadiliko ya tabianchi Wilayani Kongwa, chini ya ufadhiri wa mfuko wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi (Adaptation fund)Hayo yamebainika wakati wa ziara maalumu ya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Shirika la FECE 14 Mei 2024, wakati uwakilishi wa mataifa mbalimbali ulipotembelea miradi ya Shirika hilo ikihusisha bustani na josho la kuogeshea mifugo vilivyopo Kata ya Ugogoni.Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Machenje wakati wa ukaguzi wa josho la mifugo, Afisa Mifugo bwana Msafiri V. Mkunda alisema mradi huo umesaidia kupunguza adha kwa wafugaji na kwa Sasa Kila mifugo hulazimika kulipiwa kiasi fulani cha fedha ili kuogeshwa, na fedha hiyo hutumika kugharamia uendeshaji wa josho.
Diwani wa Kata hiyo Mhe. Elizabeth Lenjima aliipongeza Serikali kutekeleza miradi hiyo katika Kata yake kwani imesaidia kutatua baadhi ya kero zilizokuwa zikiwakabili Wananchi.Naye Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la FECE Ndugu Steven Mariki alisema wageni wamepongeza jitihada za shirika la FECE kwa kufanikisha miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi, na wapo tayari kufadhili mradi kwa awamu nyingine, kauli iliyoungwa mkono na Mratibu wa mfuko wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi bwana Faray Madziwa raia wa Zimbabwe."Licha ya Kongwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye ukame, tumefurahi kuona miradi ya kilimo cha Bustani za mbogamboga" alinukuliwa Madziwa.
Aliongeza kuwa wananchi kupitia kilimo cha umwagiliaji shamba la Chimotolo, wamezidi kuhamasika hivyo FECE sasa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa ardhi kwa ajili ya kuwezesha wananchi wengi zaidi.Kwa Mujibu wa Bwana Mariki, ziara hiyo ilihusisha wageni kutoka mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya bara la Afrika, na ni utaratibu wa Kila mwaka kwa nchi zinazonufaika na mfuko wa mabadiliko ya tabianchi kutembelea nchi moja, ambapo Tanzania imetembelewa kwa mwaka huu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.