Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amewataka wananchi wilayani humo kuacha tabia ya kuwashawishi wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha Elimu.
Dkt. Nkullo amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya sekondari Chitego unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF na wananchi wa kata hiyo.
Katika mradi huo, TASAF imetoa jumla ya shilingi 189,842,954.54 ambapo wananchi wanatarajia kuchangia nguvu kazi na vitendea kazi ambavyo ni sawa na thamani ya shilingi 12,392,000.00/= hivyo kufanya mradi kutumia jumla ya shilingi 202,234, 954.54 hadi utakapokamilika.
Kwa mujibu wa risala ya mratibu wa TASAF ndugu Elias Chilemu, miongoni mwa fedha hizo, jumla ya shilingi 20,340,316.56 zitatumika kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa nyumba hiyo yenye uwezo wa kuhudumia familia nne za walimu yaani "four in one".
Mgeni rasmi katika hafla hiyo mbunge wa jimbo la Kongwa na spika mstaafu wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai amewataka viongozi wa Kata ya Chitego kwa kushirikiana na kamati ya usimamizi wa mradi, kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha zilizotolewa na serikali ili kukamilisha mradi huo kwa ufanisi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila amesema Tatizo la la mdondoko wa wanafunzi linasababishwa na wazazi hivyo ni jukumu lao kubadilika kwa kuwaheshimu na kuwathamini Watoto wao. Ameongeza kuwa endapo viongozi na wasimamizi wa mradi huo hawatatumia vizuri fedha hizo, Halmashauri itasitisha kupeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi mingine.
Katika tukio hilo, Mbunge Ndugai amekabidhi hundi mbili kutoka Benki ya NMB zenye jumla ya shilingi 171,955,177.55 hundi ya kwanza ikiwa ni shilingi 169,502,637.98 na ya pili ikiwa na thamani ya shilingi 2,452,539.57 kwa uongozi wa Kijiji cha Chitego kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.