Na Stephen Jackson, Kongwa.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kupitia Mwenyekiti wake Mhe. White Zuberi Mwanzalila, limempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Dkt. Omary Nkullo Kutokana na utendaji wake wa kazi unaozingatia nidhamu ya Matumizi ya Fedha za wananchi.
Mheshimiwa Mwanzalila ametoa pongezi hizo wakati akihitimisha Mkutano wa Baraza la Madiwani tarehe 03 Novemba, 2021 lililoketi kupokea taarifa za Kamati za Kudumu na taarifa za Mamlaka za miji midogo ya Kongwa na Kibaigwa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Akitoa ufafanuzi Mhe. White Zuberi Mwanzalila amesema licha ya yeye mwenyewe kufanya kazi na wakurugenzi mbalimbali, Dkt. Omary Nkullo ndiye Mkurugenzi pekee ambaye hujigharamia safari zisizo za kikazi‘’. Nimefanya kazi na wakurugenzi wengi, anapokuwa na safari binafsi anajaza gari la Halmashauri mafuta linampeleka, lakini mkurugenzi wetu ya kwake binafsi anaondoka na gari yake. Ni wakurugenzi wachache mpigieni makofi’’. Amenukuliwa Mhe. Mwanzalila.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi wote kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake Dkt. Nkullo, akiwa ndiye katibu wa Baraza hilo la madiwani, amewasilisha taarifa ya Mwenyekiti ambayo inaonesha kuwa katika kipindi cha Julai-Septemba 2021, Halmashauri ilitarajia kukusanya Jumla ya TZS. 801,971,875/= na badala yake imevuka lengo kwa kukusanya TZS. 1,114,237,540.50/= Sawa na 138.9% ya lengo.
Katika baraza hilo taasisi mbalimbali zilialikwa na miongoni mwake Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira vijijini ‘’RUWASA’’ na Wakala wa barabara mijini na vijijini ‘’TARURA’’ ziliweza kuwasilisha taarifa zao kuhusu hali halisi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Meneja ‘’RUWASA’’, Mhandisi Mohamedi A. Ally, amezitaja changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na Fedha za miradi kutotolewa kwa wakati jambo linalozorotesha kasi ya uchimbaji wa visima, uhaba wa wataalamu na ushirikiano hafifu kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na chama ngazi ya jamii.
Naye Kaimu Meneja wa ‘’TARURA’’ mhandisi Boniface Mandi ameeleza kuwa awali mamlaka hiyo ilitengewa bajeti ndogo lakini kwa sasa imepandishwa hivyo matarajio ni kujenga barabara nyingi zaidi ya ilivyotegemewa. Ameongeza kuwa jumla ya kilometa mbili za lami zinatarajiwa kujengwa katika Mamlaka ya mji mdogo wa Kongwa na kilometa moja katika mji wa Kibaigwa ingawa amelishauri baraza hilo kuwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changalawe utahusika katika maeneo mengi ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wilayani Kongwa.
Mkutano wa baraza la madiwani ulioketi kupokea taarifa za Kamati za Kudumu na taarifa za Mamlaka za miji midogo ya Kongwa na Kibaigwa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka Mwaka wa Fedha 2021/2022, umefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ukihudhuriwa na Madiwani, wakuu wa Idara naTaasisi mbalimbali pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya iliyoongozana na Kaimu katibu Tawala wa Wilaya Ndugu Victor Ligate.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.