Leo tarehe 18 Septemba 2024 imefanyika ziara ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule katika wilaya ya Kongwa ili kukagua miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo. Mheshimiwa mkuu wa mkoa amesaini kitabu cha wageni katika ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ambaye pia amewasilisha taarifa ya maendeleo ya wilaya. Baada ya muhtasari wa taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Kongwa, msafara wa mkuu wa mkoa umeelekea Kibaigwa ili Kupokea taarifa na kukagua ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Afya Kibaigwa ambayo inajumuisha ujenzi wa kichomea Taka, Kondo, usimikaji wa jenereta pamoja na ukaguzi wa ujenzi wa Wodi - KOFIH.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua miundombinu ya kituo cha Afya Kibaigwa.
Akiongea baada ya kufanya ukaguzi katika kituo cha afya Kibaigwa, Mkuu wa mkoa amewaeleza wananchi kuwa muarobaini wa swala la mashine za x-ray umepatikana na mashine hizo tayari zimefika katika kituo hicho cha afya na ametoa wiki moja kwa wataalam wa kufunga mashine hizo wawe tayari wameshafunga vifaa hivyo ili mapema wiki inayofuata wananchi wapate huduma hizo katika kituo hicho cha afya. Aidha mkuu wa mkoa amegusia swala la mazingira ambayo ni sera ya kitaifa na mkoa na yeye kama mwanaharakati wa mazingira amesisitiza kuwa angependa kuona mazingira yanapendezeshwa kwa upandaji wa miti na yanatunzwa vyema katika kituo hicho cha afya kwa maana hewa safi itokanayo na mazingira nadhifu ni moja ya uponyaji.
Baada ya kutoka kituo cha afya kibaigwa msafara wa mkuu wa mkoa umesimama katika soko la Kibaigwa ambapo mkuu wa mkoa amepata wasaa wa kuwaeleza wananchi juu ya miradi iliyotekelezwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo wodi ya wanaume ambayo ilikuwa ombi maalum kutoka kwa wananchi. Aidha mkuu wa mkoa amesikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu na pia kuwahimiza wajitokeze kwa wingi kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kuhakiki taarifa zao na wale ambao watatimiza miaka 18 wakaandikishe taarifa zao ili ifikapo wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, wapate nafasi ya kushiriki zoezi hilo ambalo ni haki kikatiba.
Msafara wa mkuu wa mkoa pia umewasili katika shule ya Dkt Omary Nkullo ili Kupokea taarifa na Kukagua Ujenzi wa vyumba 9 vya madarasa na matundu 8 ya Vyoo katika shule hiyo ambapo mkuu wa mkoa ameelezea dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuleta madarasa hayo ni kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa katika mazingira mazuri na salama kwa kusudio la kuongeza ufaulu ili miaka ijayo wapatikane wataalam wenye maarifa na ujuzi wa kuweza kuendeleza nchi yao katika Nyanja mbalimbali ikiwemo sayansi na teknolojia. Aidha wadau mbalimbali ikiwemo walimu wameaswa kufanya kazi kwa bidii kwa kufundisha na kuhimiza wazazi na wanafunzi kutokomeza swala la utoro shuleni ili kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kwa maendeleo ya taifa.
Mkuu wa Mkoa wa dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wanafunzi wa shule ya Dkt Nkullo.
Aidha msafara wa mkuu wa mkoa umeelekea zahanati ya Ngomai kukabidhi kiwanja, saruji mifuko 65 na kuchimba msingi wa nyumba ya Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Kijiji cha Ngomai ambapo wananchi wa Ngomai waliamua kumnunulia kiwanja Mganga mfawidhi kama shukrani kwa utumishi wake mzuri uliotukuka. Baada ya kukabidhi kiwanja, mkuu wa mkoa amepata wasaa wa kumpongeza Mganga mfawidhi daktari Peter kwa kazi yake nzuri iliyopelekea kuzawadiwa kiwanja hicho na wananchi na kuwaasa watumishi wengine wa serikali waige mfano mzuri wa utendaji kazi na uadilifu kutoka kwa daktari Peter kwani wananchi wanaona na wanatambua kazi nzuri ikifanywa na mtumishi wa umma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akimkabidhi Daktari Peter kiwanja alichonunuliwa na wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemalizia ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ngomai ambapo umati wa watu umefika kumsikiliza na baadhi yao kutoa kero zao ambazo zimepatiwa majibu kikamilifu na wataalamu walioambatana naye. Akifungua hotuba yake mkuu wa mkoa amewashukuru wananchi wa Ngomai kwa mapokezi mazuri ya ngoma na kwaya aliyoyapata na kuonyesha furaha yake kwa jumbe zilizokuwa zimeambatana na mashairi mazuri. Aidha mkuu wa mkoa ametoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Ngomai na kuwaeleza wananchi juu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya ya Kongwa na kuwa serikali inafanya kazi ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.
Ziara hii ni muendelezo wa ziara za kikazi za Mheshimiwa Rosemary Senyamule katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Dodoma ili kukagua miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea utatuzi pamoja na kusambaza ujumbe kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litakaloanza tarehe 25 Septemba na kutamatika tarehe 1 Oktoba mwaka huu.
Karibu tena wilaya ya Kongwa mheshimiwa Rosemary Senyamule.
Imeandaliwa na;
Mbonea E. Masha
Afisa Habari wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.