Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka amewahimiza akina baba kubeba na kulea watoto wao kwani malezi ni ya pande zote mbili na kitendo hicho hakiondoi maana na thamani ya baba bali kinaongeza thamani ya baba katika familia.
Mhe. Mayeka ameyasema hayo jana alipokuwa katika maadhimisho ya siku ya Afya na lishe yaliyofanyika katika Kata ya Sagara Kijiji cha Msingisa na kuhudhuriwa na wananchi, wataalam pamoja na mashirika wadau wa lishe ambapo mhe. Mayeka amebainisha kuwa ulinzi wa familia huanza na chakula Pamoja na malezi bora, lakini wanaume wengi wamekuwa wakikwepa kulea watoto wakidhani kwamba kulea ni jukumu la mama peke yake.
Aidha DC. Mayeka ameongeza kuwa suala la lishe ni suala muhimu sana kwani husaidia kujenga kinga ya mwili hivyo swala hilo halipaswi kuchukuliwa kirahisi kwani linaweza kupelekea Serikali kupata mzigo mkubwa kununua madawa kwaajili ya kutibu maradhi ambayo mengi husababishwa na ukosefu wa lishe bora.
Licha ya kuhimiza umuhimu wa siku ya Afya na lishe ya kijiji kufanyika mara kwa mara katika Kila Kijiji lakini pia Mhe. Mayeka amehimiza wazazi kuwapatia watoto muda wa kucheza, kupumzika na kuhakikisha wanazingatia lishe bora mara wanapofikisha miezi sita tangu kuzaliwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amesisiza malezi ya watoto na amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Msingisa kwa mabadiliko makubwa katika elimu, yaliyochangiwa na hatua ya wanakijiji kuajiri walimu wa kujitolea kufundisha watoto wao na kuwataka kuongeza juhudi hiyo katika suala la utekelezaji wa shughuli za Afya na lishe kijijini.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za afya na lishe za Halmashauri, Afisa lishe wilaya ya Kongwa, Bi Mary Haule amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa watu 75,895 ni watoto chini ya miaka mitano ambapo 31% ya watoto walio chini ya miaka mitano wamedumaa sawa na watoto 23,537. Ameongeza pia kuwa 14% ya watoto chini ya miaka 15 wana uzito pungufu sawa na watoto 10,625 na katika kipindi cha mwaka 2024 watoto 149 walitibiwa utapiamlo mkali.
Aidha, Bi Haule amesema kuwa Halmashauri inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza afua za lishe kwa kutoa elimu ya lishe kwa wananchi kuzingatia mtindo bora wa lishe kwa kuzingatia makundi sita ya vyakula , kuhimiza umuhimu wa kuepuka mtindo bwete Kwa kufanya mazoezi, kuhimiza mbinu bora za kilimo na utunzaji mazao, kutoa huduma za malezi ya Watoto, kupeleka watoto shule na kuwapatia lishe za unga wenye virutubisho.
Vilevile Bi Haule amezitaja changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa masuala ya lishe kuwa ni ushiriki duni wa wanaume katika shughuli za afya na lishe, wajawazito kuchelewa kuanza kliniki chini ya wiki 12, idadi ndogo ya wanafunzi wanakula shuleni kutokana na wazazi kutokuchangia chakula, idadi ndogo ya mashine zilizofungwa kifaa cha kuongeza virutubishi Pamoja na ukosefu wa fedha kwaajili ya kuendeshea siku ya afya na lishe kijijini.
Katika maadhimisho hayo huduma mbalimbali zilitolewa zikiwemo huduma za upimaji virusi vya ukimwi, uchunguzi wa Magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, huduma za lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, kilimo na usalama wa chakula, elimu ya unawaji wa mikono na elimu ya mapishi ya vyakula mchanganyiko kwa watoto, wajawazito na wanaonyonyesha ili kusaidia kuleta nguvu na kukuwa kirahisi ambapo maadhimisho hayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.