Baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliopelekea kupatikana kwa viongozi ikiwemo wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji, wajumbe wa halmashauri za vijiji mchanganyiko Pamoja na makundi maalimu. Viongozi walioshinda wamepata fursa ya kupatiwa semina ya mafunzo iliyokuwa na mada mbalimbali ili kuwawezesha kufanya majukumu yao kwa ufasaha.
Mgeni rasmi wa semina ya mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka akifungua semina za mafunzo hayo kwanza amewapongeza viongozi waliochaguliwa ili kuwatumikia wananchi na kuwasihi kuwa ushirikiano wao ni muhimu ili wananchi wapatiwe huduma muhimu kwa wakati na kero zao zitatuliwe kwa muda mfupi sana.
Mhe. Mayeka pia amewaeleza viongozi hao kuwa wao ni kiunganishi muhimu cha serikali na wananchi kwani wao ndio wako karibu sana na wananchi na wanajua wanayoyapitia wananchi kwa ukaribu sana na utatuzi wa maswala mbalimbali unaanza nao.
Aidha mhe. Mayeka amewasihi viongozi hao kufata taratibu zote za uongozi na maswala watakayofundishwa na wasijiingize kwenye matendo maovu yatakayochafua uongozi wao Pamoja na vyama vyao vya siasa ambavyo vimewaamini na kuwapa dhamana ya kutekeleza ilani ya vyama husika.
Akiongea wakati akimkaribisha mgeni rasmi, mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omar Nkullo amewashukuru viongozi hao kujitokeza kwa wingi na umoja wao katika mafunzo hayo na kuwasisitiza kuwa umoja huo ndio utakaofanikisha maswala mengi ya kimaendeleo katika maeneo yao ya uongozi.
Baadhi ya mada zilizotolewa kwa viongozi katika semina ya mafunzo ni Pamoja na Sheria za Uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazokuwa ni muongozo muhimu ili kusaidia viongozi kutekeleza shughuli zao za kila siku.
Mada nyingine ni Pamoja na Muundo, Majukumu na Madaraka ya Vijiji na Vitongoji Pamoja na Uongozi na Utawala bora, ambayo ni mambo muhimu viongozi kuelewa wakati wanapoelekea kutekeleza majukumu yao ya uongozi.
Viongozi pia wamefunzwa kuhusu uendeshaji wa Vikao na Mikutano katika Ngazi za Vijiji na Vitongoji sababu elimu ya kuendesha vikao ni nguzo muhimu itakayowasaidia kuitisha vikao vinavyojadili ajenda tofauti tofauti ikiwemo ajenda za maendeleo ya vijiji na vitongoji, pia viongozi wamefunzwa kuhusu Uibuaji, Upangaji na Usimamizi wa Miradi Shirikishi ya Kijamii Pamoja na usimamizi na Udhibiti wa Fedha katika Mamlaka za Serkali za Mitaa.
Aidha mada nyingine muhimu zilizowasilishwa kwa viongozi ni Pamoja na Usimamizi wa Ununuzi Pamoja na Usimamizi wa Aridhi na Udhibiti wa Uendelezaji Vijiji.
Viongozi waliopatiwa mafunzo wameahidi kuyatumia vizuri mafunzo hayo ili kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku katika nyadhfa zao kwa madhumuni mapana ya kuwaletea wananchi maendeleo na kutatua changamoto zitakazojitokeza katika maeneo yao ya uongozi
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.