"Tuwatambue wageni katika maeneo yetu" - DC Kongwa
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Saimon Mayeka amewaasa viongozi wa Kata kutoa elimu na kuzungumzia zaidi suala la ulinzi na usalama kwa Wananchi ili kuwatambua wageni ambao hawatambuliki katika maeneo yao na kuwatolea taarifa zitakazosaidia kuwatambulisha na wasisubiri matukio ya uhalifu yatokee ndipo umuhimu wa taarifa za kuwatambua wageni uonekane.
Mheshimiwa Mayeka ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la madiwani wa kujadili taarifa za maendeleo ya Halmashauri kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 uliohudhuriwa na madiwani wa kata zote, viongozi wa serikali na vyama vya siasa pamoja na wataalam wa idara na taasisi mbalimbali.
Ameongeza na kusema kuwa hali ya ulinzi na usalama sio mbaya japokuwa kuna shida ya simba waliokuwa wakitembea katika maeneo mbalimbali ya wilaya ambao wameleta taharuki hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuacha kutembea usiku katika maeneo yenye mapori.
Aidha Mheshimiwa Mayeka amesisitiza suala la usafi wa mazingira kwa kuwasihi madiwani wawaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa usafi wa mazingira ili kuwasaidia maafisa afya katika kazi zao, pia amewaasa wananchi waache kulima mazao marefu kama mahindi katikati ya viunga vya miji ili kupendezesha miji isiendelee kuonekana kama vijiji. Mheshimiwa Mayeka amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanahimizwa kupanda miti na kuacha kulima milimani ili kulinda uoto na mandhari ya milima.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.