Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi amezindua kampeni ya Kutokomeza Ndoa za Utotoni Wilayani Kongwa inayosimamiwa na Shirika la World Vision linalofanya kazi katika Tarafa ya Zoissa, Kata za Mkoka, Makawa na Matongoro.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika jana atrehe 23 - 01 - 2018, Mhe Ndejembi aliwahimiza wasimamizi wa mradi huo kujikita zaidi kwenye kutoa elimu katika jamii ili kuondokana na mila kandamizi. Aidha, amewataka wazazi na walezi kutowabagua watoto wao bali wawalee katika misingi ya usawa kwa kutoa haki sawa kwa watoto wote, wa kike na wa kiume ikiwemo haki sawa ya kupata elimu, kwani kuna baadhi ya wazazi bado wanaamini watoto wa kike ni kwa ajili ya kuolewa na wa kiume ni kwa ajili kurithi mali.
Pia, Mhe DC amewataka wenyenyeji (kabila la wagogo) waachane na mambo ya ndima katika kusimamia haki za mtoto wa kike pindi inapotokea kwamba kuna mtoto ametendewa visivyo, sheria ifuate mkondo wake na jamii ishiriki kikamilifu katika kutoa utetezi mahakamani
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Mhe. White Zuberi, aliwahimiza Wakuu wa Idara na Vitengo kuutumia vyema elimu iliyotolewa katika uzinduzi wa kampeni hiyo na kuwataka waisambaze kwa watendaji waliopo chini ya idara zao katika kufikisha ujumbe kwa wananchi wote.
Aidha, Mwenyekiti amewakaribisha waendesha kampeni hii (Shirika la World Vision) katika mkutano wa Baraza utakaofanyika mwisho wa mwezi huu kufika kutoa elimu kwa madiwani ili wakatumike katika kata zao kusambaza elimu ya kutokomeza mimba za utotoni wilayani Kongwa.
Pia, Mwenyekiti, amewaomba wasimamizi wa mradi wasijikite katika eneo dogo la kata tatu (3) tu, na badala yake wapanue mradi na kufikia maeneo mengine ya wilaya ya Kongwa katika tarafa zote tatu.
Mwishowe, washiriki wa uzinduzi huu wa kampeni ya kutokomeza ndoa za utotoni wilayani Kongwa kwa pamoja wameazimia kwamba elimu itolewe kwa wananchi wote kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na pia, katika kila mkutano na wananchi ndani ya wilaya ya Kongwa katika ngazi zote “Elimu kuhusu Madhara ya Ndoa za Utotoni” iwe agenda kuu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.