Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote – UCSAF Atembelea Kongwa
Imewekwa: September 7th, 2021
Mtendaji Makuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba leo tarehe 7 Septemba, 2021 amefanya ziara Wilayani Kongwa. Katika ziara hii emeambatana na wawakilishi wa makampuni ya simu ya TTCL, Airtel, Halotel, Tigo na Vodacom katika Mkoa wa Dodoma.
Ziara hii imeongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai kutembelea maeneo ya Kata za Kongwa katika mtaa wa Mnyakongo, Sagara – vijiji vya Sagara B na Laikala, Mtanana - eneo la Ranchi ya Taifa ya NARCO, Hogoro kijiji cha Chamae na Sejeli kijiji cha Msunjilile ikiwa ni uwakilishi wa maeneo yote yenye changamoto ya mawasiliano hafifu katika Wilaya ya Kongwa.
Lengo kuu la ziara hii ni kutembelea baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto za mawasiliano Wilayani Kongwa ili wawakilishi wa kampuni za simu waweze kujionea wenyewe hali halisi ya changamoto jinsi ilivyo na kuona namna ya kutatua changamoto katika maeneo hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius M. Emmanuel akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ameshiriki ziara hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Serikali – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kwamba huduma za mawasiliano zinapatikana kwa lengo la kuchohea uchumi wa wananchi.
Mapema Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Bw. Nkinde Moses aliwasilisha taarifa ya hali ya mawasiliano Wilayani Kongwa kwa ufupi ambapo ameeleza kuwa Wilaya ya Kongwa ina minara ya simu 36 katika kata 19 na ni kata 3 tu ambazo hazina minara. Kata ambazo hazina minara kabisa ni Chitego, Hogoro na Makawa zinazopata mawasiliano kutoka minara ya kata zingine na kupelekea mawasiliano kuwa hafifu. Aidha, ameeleza kwamba pamoja na uwepo wa minara hiyo, baadhi ya maeneo yamekuwa na mawasiliano hafifu kwa upande wa data kwani teknolojia inayotumika ni ya kizazi cha pili (2G) inayowezesha mawasiliano ya sauti tu na mengine 3G inayowezesha data kwa kiwango cha chini.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary A. Nkullo ameeleza kwamba changamoto ni kubwa sana ukizangatia kwamba Serikali inatoa huduma kwa njia ya kidijitali kupitia mifumo ya TEHAMA amemuomba Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote - UCSAF kuwezesha uboreshaji wa mawasiliano katika maeneo ya vijijini kwenda vizazi vya 3G na 4G ili kuboresha huduma za data. Kwa sasa Halmashauri imewekeza mashine za kukusanyia mapato (POS) ambazo zinazotumia mawasiliano ya data kufikisha taarifa kwenye Mfumo Mkuu wa LGRCIS, hivyo, huduma hafifu za data kumepelekea kuwa na shida ya kupata taarifa kutoka kwa wakusanyaji na kuingia gharama ya usafiri kwa wakusanyaji kwenda maeneo mengine yenye mawasiliano mazuri ya data ili kutuma taarifa.
Aidha, Dkt. Omary A. Nkullo ameomba Mfuko huu utilie mkazo katika kuboresha mawasiliano ya sauti na data katika eneo la Makao Makuu ya Wilaya hususani eneo la Mnyakongo - Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo watumishi wengi wanaishi wakiwemo Wakuu wa Idara na Wakuu wa Taasisi zilizopo Wilayani Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Remidius M. Emmanuel ameeleza kwamba kumekuwa na changamoto za baadhi ya watumishi wa makampuni ya simu wamekuwa wakichukua maeneo wanayoona yanafaa kwa ajili ya uwekaji wa minara na kujimilikisha na kuleta migongano na wananchi. Hivyo, uongozi wa Wilaya kupitia Halmashauri imeunda timu inayofuatilia mikataba yote ya minara ili kuona namna ya kuingia upya mikataba hiyo. Ameeleza pia, kuwa Meneja wa TTCL Mkoa wa Dodoma amethibitisha kwamba mnara wa kijiji cha Chang’ombe kata ya Iduo hadi kufikia mwezi Desemba utakuwa na huduma za 4G barua ameshawasilia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuhusu kusudio la utekelezaji huo.
Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai wakati akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano ameyataja baadhi ya maeneo kama vile Sagara, NARCO, Chamae na Msunjilile kuwa yana changamoto za mawasiliano, na kugusia kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana Wilayani Kongwa katika upande wa redio kiasi kwamba kusikiliza redio imekuwa taabu sana. Aidha, amemuomba sana, sana, sana Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuyaangalia maeneo hayo, lakini pia pamoja na mengine ya yaliyotajwa kwenye taarifa ya Afisa TEHAMA.
Mwisho, Mtendaji Makuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba amesema amefurahi sana kufika Kongwa na kusema kwenye Wilaya ya Kongwa kuna miradi 2 tu mmoja wa Vodacom Kata ya Njoge na wapili wa TTCL kijiji cha Chang’ombe Kata ya Iduo, kwa mradi wa Njoge wameshaingia mkataba na Vodacom kuuboresha kwenda 4G hadi kufikia mwezi Desemba kazi itakuwa imekamilika.
Aidha, Bi Justina, ameeleza kwamba hivi karibuni zitangazwa zabuni na kata zilizotajwa pamoja na Kongwa Mjini zitaingizwa kwenye miradi ya hivi karibuni. Pia, Wataalam watapita kufanya majaribio ya kuona nini shida, na kisha kumuomba Afisa TEHAMA amuwasilishie taarifa ya kina kuhusu mchanganuo wa maeneo yenye changamoto ya mawasiliano kwa ngazi ya vijiji na vitongoji ili Mfuko uyafanyie kazi kwa kushirikiana na makampuni ya simu kwani kwa sasa Mfuko umeshaachana na Kata unaenda kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji.