Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Mwenyekiti wa kijiji cha Mlanje kilichopo Kata ya Matongoro Wilayani Kongwa Ndugu Elisha Njingu Mpanda amerejeshwa madarakani baada ya Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kutokubaini hatia yoyote dhidi yake.
Hatua hiyo imekuja hivi karibuni baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Mayeka Simon Mayeka kufika katika Kata ya Matongoro kwa lengo la kumrejesha madarakani mwenyekiti huyo aliyekuwa anakabiliwa na kosa la kusababisha vurugu kwa wananchi kwa kuuza eneo la kijiji lililotengwa kwaajili ya malisho.
"Mwenyekiti wa kijiji cha Mlanje atarudishwa madarakani ili aendelee na majukumu yake lakini mwenyekiti wa kijiji cha Matongoro bado anaendelea na kesi yake mahakamani kwa kuwa uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa ana hatia". Alisema Mayeka.
Aidha Mhe. Mayeka amefafanua kuwa katika mgogoro ule mwenyekiti wa kijiji cha Mlanje alirubuniwa na Mwenyekiti wa kijiji jirani cha Matongoro ili wauze eneo la kijiji lililotengwa kwa ajili ya malisho na kuwauzia wakulima wa kijiji cha Matongoro ambapo mpaka wakati huu eneo hilo lililokuwa na hekari 12,000 kwa limebaki na hekari 2,000.
Akiongea mbele ya mkutano wa hadhara mwenyekiti wa kijiji cha Mlanje ndugu Mpanda amesema anashukuru uongozi wa Wilaya Kongwa na ofisi ya TAKUKURU kwa Uchunguzi walioufanya na kubaini ukweli na ameahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za uongozi wa Serikali za mitaa ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu na kufanya shughuli zao za maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mlanje akiwa pamoja na Mwenyekiti wa kijiji cha Matongoro walisimamishwa kazi mnamo Februari 2025 kwa kosa la kushirikiana kuuza maeneo ya ardhi ya Vijiji hivyo kwa maslahi yao binafsi na kusababisha mgogoro wa mpaka baina ya Vijiji hivyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.