Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony Mavunde amezindua rasmi kampeni ya upandaji miti Wilayani Kongwa jana, Januari 25, 2018 katika maeneo ya chini ya safu ya milima Kiboriani eneo la Kijiji cha Ibwaga.
Katika uzinduzi huo, Mhe Mavunde amewataka wananchi wa Kijiji cha Ibwaga kuleta mabadiliko ya kifikira katika kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa wa kijani kwa kupanda miti na kutunza mazingira ili kuongeza fursa za kiuchumi ikiwemo za kilimo na ufugaji wa nyuki.
Mhe Mavunde amewataka wananchi hao wajitolee kuunda vikundi vya utunzaji wa mazingira ili viweze kufaidika na Mfuko wa Misitu Tanzania Forest Fund (TFF) unatoa ruzuku ya utunzaji wa misitu ili kuweza kujiinua katika fursa za kiuchumi ikiwemo ufugaji wa nyuki na katika mazingira hayo wanayoyatunza.
Aidha, aliwataka kutambua kwamba mkoa wa Dodoma ndio mkoa wa kipekee wenye ardhi inayokubali mazao tofautitofauti likiwemo zao pekee la zabibu ambalo ulimwenguni kote hilo likilimwa mkoani Dodoma huvunwa mara mbili kwa mwaka, hivyo utunzaji wa mazingira utawezesha fursa ya kilimo kuboreshwa. Mhe Mavunde alisisitiza kwa kusema “Nitajisikia huzuni sana kama zoezi hili halitafika mwisho na mwisho wa zoezi hili ni kuifanya Kongwa kuwa ya kijani”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi ameeleza masikitiko yake kuhusiana na hali ya uharibifu wa mazingira wilayani Kongwa unaotokana na shughuli za kilimo na uchomaji wa mkaa na kuwataka wananchi wote kuthamini na kutunza mazingira.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mazingira (W), Bw. Godfrey Mujairi alisema katika uzinduzi huo itapandwa miti zaidi ya 1000 kando ya milima kijijini hapo na wanatarajia kupanda miti milioni 1.5 wilaya nzima. Na zoezi hili la upandaji miti litaambatana na kutunza visiki hai ili kufufua uoto wa asili pia miti inayostahimili hali ya ukame ndiyo waliyoichagua ikiwemo; mikungugu, mikorosho, mitimaji, panga uzazi na mimelea na upandaji huo umelenga kipindi cha mvua za Masika.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.