Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Angelina Mabula amezungumza na Wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa kuhusu Migogoro ya Ardhi kama sehemu ya utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa Tarehe 07/07/2021.
Awali Kiongozi huyo aliwasili katika ukumbi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kiabaigwa na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama na kisha kufanya kikao cha ndani na viongozi mbalimbali wa mamlaka hiyo, pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Lengo kubwa la kikao hicho lilikuwa ni kutambua hali halisi ya Migogoro iliyopo, vyanzo vyake na Hatua zilizochukuliwa kutatua Migogoro hiyo.
Baada ya kikao hicho, Naibu waziri Mhe. Angelina Mabula aliongozana na Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Mwema Emmanuel na kamati ya ulinzi na usalama na wajumbe wote wa kikao hicho kuelekea katika kiwanja cha michezo cha Mamlaka ya Mji wa Kibaigwa na kufanya mkutano wa Hadhara na Wananchi.
Katika mkutano huo, kero zipatazo thelathini na tisa (39) ziliwasilisha mbele ya Naibu Waziri huyo ambazo kati yake nyingi zilijibiwa na timu ya wataalamu kutoka Idara ya Ardhi na Viongozi wa mamlaka ya Mji Mdogo Kibaigwa wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Dr. Omary Mkullo.
Akihutubia Mkutano huo Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula, ametoa Elimu ya kutosha kwa wananchi hao kuhusu Taratibu za kupimiwa na kumilikishwa Ardhi na jinsi ya kushughulikia kero za ucheleweshwaji wa Mashauri ya Migogoro ya Ardhi yaliyopo Mahakamani au katika mabaraza ya Ardhi.
Katika mazingira hayo, amewashauri Wananchi Kufika ofisi za wasajili wa Mahakama au Mabaraza husika ili watoe malalamiko yao. Na kwa wale wanaopata ushindi katika ngazi yoyote ya Maamuzi, wameelekezwa kufika ngazi zinazohusika na kukazia Hukumu zao ili kusaidia utekelezaji wa maamuzi hayo.
Ili kupunguza Migogoro ya Ardhi Mhe. Naibu waziri amewataka wananchi kuthamini Ardhi na kuzitambua gharama halisi za kupimiwa na kumilikishwa Ardhi. Hivyo ametoa maagizo mbalimbali kwa wataalamu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri.
Miongoni mwa Maagizo hayo ni pamoja na Wataalamu wa Ardhi kuhakikisha wanazingatia taratibu zote za upimaji Ardhi ikiwa ni pamoja na kushirikisha majirani wote wanaopakana na Ardhi inayopimwa wakati wa upimaji ili kuepusha migogoro ya baadaye, kuhakikisha Taasisi zote za umma zinapimiwa Ardhi na kupewa Hati Milki na kuwatembelea wananchi na kuwapa Elimu kuhusu matumizi bora ya ardhi na taratibu za kupimiwa na kumilikishwa.
Ameongeza kuwa zoezi la urasimishaji linafanyika kwenye maeneo yaliyojengwa kihorela na litaishia mwaka 2023, hivyo Serikali haihusiki na fidia kwa mwananchi ambaye eneo lake linapitiwa na Miundombinu ya huduma za jamii.
Naye kamishina wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Kabonge alipata nafasi ya Kuzungumza na Wananchi hao na kusema kama viongozi wa Mkoa watafika Kibaigwa kwa mara nyingine kusikiliza migogoro midogo midogo ya Ardhi, na kutoa hati za kielectroniki kwa wananchi waliokidhi vigezo. Lakini wakakti huo huo amewasisitiza wananchi wanaomiliki ardhi kulipa kodi ya Ardhi.
Ili kuondoa kero za Mpangilio wa Mji wa Kibaigwa, Kamishna wa Ardhi Mkoa, Ameahidi kuwa kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya kongwa utaandaliwa Mpango kabambe wa kuboresha Mji huo wa kibiashara ambao wananchi watatakiwa Kuuheshimu.
Mkutano huo wa Hadhara uliohudhuriwa na Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Kamishina wa Ardhi mkoa wa Dodoma viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Kongwa na mamlaka ya Mji mdogo wa Kibaigwa umeonekana kuwavutia sana Wananchi wa Kibaigwa.
Stephen Jackson - Kongwa
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.