Shirika la Nature Tanzania linalotekeleza Mradi wa kupunguza mauaji ya ndege aina ya Korongo weupe katika wilaya ya Kongwa na Mpwapwa limegawa mbuzi 25 kwa vikundi viwili vinavyotoka katika Kijiji cha Manungu na Morisheni katika Wilaya ya Kongwa. Huu ni muendelezo wa mradi wake wa kupunguza mauaji ya ndege hao ambapo tathmini imeonyesha kuwa kati ya ndege 500 hadi 1000 huuwawa kila mwaka katika msimu wa masika.
Licha ya kutoa mbuzi pia Nature Tanzania imeendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na ndege kwani ndege hawa husaidia kula wadudu waharibifu wa mashambani kama vile panzi na viwavijeshi.
Meneja wa Mradi kutoka Nature Tanzania Bi. Neema Mwaja, ameeleza katika risala kuwa shirika pia limefanikiwa kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa wanufaika 60 kwa kushirikiana na TFS ambapo wamegawa mizinga 30 ya kisasa katika vijiji mbalimbali wilayani Kongwa ikiwemo Mlanga, Morisheni Manungu na pia shirika limegawa vifaa vya kuvunia asali ikiwemo mavazi, viatu, mashine ya kuchakata na kuchuja asali, ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa wanufaika kwa dhumuni la kukuza Uchumi wao.
Akizungumza kabla ya kushiriki zoezi la kukabidhi mbuzi hao, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka akiongea na wananchi amesisitiza ufugaji wenye tija na kueleza kuwa kutegemea kilimo vipindi ambavyo mazao hayajafanya vizuri ni hatari kwani chakula kinapokosekana, watu huingia katika uwindaji holela ikiwemo uwindaji wa ndege hao ili kusudi wapate vitoweo.
Mhe. Mayeka ametolea mfano nchi ya Sudan ambayo jamii kubwa ni wafugaji na kueleza kuwa Kongwa ikijikita katika ufugaji wenye tija, basi inawezakuuza mifugo na kulilisha jiji la Dodoma na kufanya Kongwa kuwa kitovu cha biashara ya Mifugo na kuongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa chanjo kwa wafugaji ili kupambana na magonjwa ya mifugo kwa dhumuni la kuwezesha wafugaji kunufaika na biashara hiyo sababu chanjo zimepunguza magonjwa ya mifugo kwa kiasi kikubwa sana.
Akiongea kwa niaba ya wanakikundi walionufaika na mradi, mwenyekiti wa kikundi kutoka Kijiji cha Manungu ametoa shukrani zake za dhati kwa shirika la Nature Tanzania na kuahidi kuwa mbuzi hao watasimamiwa kwa umakini ili wazaliane na kukwamua Uchumi wa familia zao na jamii kwa ujumla. Ameongeza kuwa usimamizi mzuri wa mifugo hiyo utafanya jamii iwe na chakula cha kutosha, fedha zitokanazo na biashara ya mifugo, maendeleo ambayo yataiondoa jamii katika uwindaji wa ndege aina ya Korongo weupe kwa ajili ya kitoweo.
Mradi huu unakuja baada ya utafiti kuonyesha kuwa ndege hawa huuliwa kwa sumu na huuzwa kati ya shilingi 2500- 5000 hivyo kufanya Nature Tanzania kushiriiana na NABU international Foundation kuanzisha mradi wa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwatafutia njia mbadala za kuwapatia kipato ikiwemo ufugaji wa nyuki, ufugaji wa mbuzi na ufugaji wa kuku pamoja na kutoa elimu juu ya uhifadhi ndege vijijini na mashuleni ili kupunguza mauaji ya ndege hao.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.