Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kutumia fedha wanazopewa kuinua kipato na kuboresha Maisha yao badala ya kuzitumia kwa anasa.“Fedha hizo mnazozipata kupitia TASAF sio za kufanyia anasa bali zinatakiwa zitumike katika masuala ya maendeleo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuboresha maisha yenu,” Alisema Mhe. Ndejembi.
Mheshimiwa Ndejembi amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ugogoni katika Kata ya Ugogoni Wilayani Kongwa Novemba 10, 2021.
Katika hotuba yake alieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita imeamua kuingiza vijiji vyote kwenye mpango wa TASAF ili kuinua hali ya Maisha ya wananchi. Aidha, ametoa rai kwa wanufaika wa TASAF kuzitumia Fedha wanazozipata kufanyia shughuli zinazolenga kuwaongezea kipato kama vile kilimo na ufugaji wa kisasa.
Kufuatia hotuba hiyo, Mratibu wa TASAF Wilayani Kongwa, Ndugu Elias Chilemu, alitolea ufafanuzi kuwa wanufaika wasiohakikiwa na kupelekea kukosa malipo kwa awamu mbili mfululizo mfumo wa malipo unaweza kuwaondoa, hivyo ili kurejeshwa kwenye malipo hayo wanaweza kuhakikiwa na pia kujaza fomu maalumu za madai.
TASAF Wilaya ya Kongwa inahudumia jumla ya kaya 7,821 ambapo kati yake kaya 170 hazikuhakikiwa katika zoezi la uhakiki la Mwezi Agosti, 2020 kwa sababu mbalimbali zikiwemo kuhama katika maeneo ya utekelezaji na wengine kutohudhuria katika zoezi hilo kwa sababu mbalimbali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amemuhakikishia kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa TASAF katika vijiji vyote themanini na saba (87) vya Wilaya ya Kongwa kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyowasilishwa kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, Uongozi wa Wilaya ya Kongwa umetoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya sita kwa kutoa ruzuku ya kiasi cha Tsh 10,023,792,911.08 kama ruzuku ya kutimiza masharti ya afya na elimu pamoja na mradi wa Timiza Malengo, kupitia TASAF III.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.