Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yametakiwa kudumisha ushirikiano mzuri baina yao na Serikali kwa kuhakikisha yanakuwa na muamko katika kushiriki shughuli za Serikali Pamoja na kuishirikisha Serikali katika matukio yao mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka katika kikao na Mashirika yasiyokuwa yakiserikali (NGO’S) na wadau wengine wa maendeleo ili kupokea na kuthibitisha taarifa za utekelezaji wa miradi inayofanywa na Mashirika hayo ndani ya Wilaya ya Kongwa.
Aidha, Mhe. Mayeka amesisitiza kuwa suala la matumizi ya nishati safi lipewe kipaumbele ili kulinda mazingira na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr Samia Suluhu Hassan. Aidha Mgeni rasmi amesisitiza kila shirika kuweka mpango wa usambazaji na upandaji miti katika maeneo ya Wilaya ya Kongwa ili kuboresha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mashirika yasiyokuwa yakiserikali yametumia kikao husika ili kusudi kueleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao. Shirika LA SATF (Socal Action Trust Fund) limeeelezea changamoto wanayokutana nayo kuwa wanafunzi wengi ambao wamekuwa wakiwasaidia vifaa vya shule wanakuwa watoro, hii inapelekea wanafunzi hao kuacha shule na shirika hilo limetumia wasaa huo kuomba mamlaka husika za Serikali kushughulikia changamoto hiyo ili misaada wanayotoa iwe na tija kwa wanafunzi na changamoto ya utoro ipatiwe ufumbuzi ili wanafunzi wamalize masomo yao.
Aidha changamoto nyingine iliyoibuliwa ni pamoja na kukithiri kwa utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano licha ya juhudi za mashirika kutoa misaada ya chakula pamoja na lishe. Imegundulika kuwa wazazi wengi hawana muda wa kuzingatia ulaji sahihi wa watoto wao na kutotilia mkazo jukumu hilo hali inayopelekea utapiamlo kukithiri.
Kwa upande wake Bwana Omary Msenga kutoka Shirika la THF linalohusika na kilimo cha umwagiliaji ameeleza kuwa vijana wengi wanaolima Kilimo cha umwagiliaji wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji, ushuru uliokithiri katika usafirishaji wa mazao na vipimo gandamizi vya mazao yao na kutumia nafasi yake kuomba mamlaka husika kushughulikia changamoto hizo.
Kwa upande wake muwakilishi wa shirika lisilo la Kiserikali la ‘Kizazi Hodari’ Bi Nasra Abubakar ameelezea changamoto ya wanaume wengi kuendelea kuwa nyuma katika jukumu la malezi ya Watoto huku akieleza kuwa changamoto hii inachangia wazazi wengi kutokuwafatilia watoto wanaoishi na VVU katika matumizi ya dawa.
Akichangia mada katika kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kongwa, Bi Faraja Kasuwi amewataka vijana kujikita katika Kilimo cha umwagiliaji na kuongeza kuwa Mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inatolewa kwa vikundi vinavyojishughulisha na miradi ya maendeleo kwa ajili ya kukuza mitaji na kuinua kipato cha wananchi.
Akiongea wakati wa kufunga kikao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dr Omary Nkullo ameyashukuru mashirika yote yasiyokuwa yakiserikali kwa kuiunga mkono Serikali na kusaidia jamii.
Sambamba na hayo Dr Nkullo ameagiza Idara ya Kilimo kwa kushirikiana na Watendaji wa Vijiji kufatilia na kuliweka sawa suala la vipimo vya mazao na ushuru kandamizi wa wakulima wa mazao ya biashara.
Baadhi ya mashirika yasiyokuwa yakiserikali yaliyoshiriki mkutano huo ni pamoja na LVIA, Lead foundation, Ufundiko, World Vision, Cuamn, Bizy Tech, Mviwata, Tahea, Sat na Emap.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.