Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SA CP George Katabazi amewataka maafisa Polisi wa Kata Wilayani Kongwa kuishi ndani ya Kata wanazozisimamia ili kusaidia kubaini changamoto za raia wanaowasimamia
Kamanda Katabazi ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi alipotembelea Wilaya ya Kongwa ili kuongea na maafisa wa Polisi na Watendaji Kata juu ya kudumisha ushirikiano baina yao katika kuleta amani na utulivu wa maeneo wanayoyaongoza ambapo sambambsa na hilo ametoa wiki mbili kuhakikisha kila Polisi kata anahamia katika Kata yake.
Aidha Kamanda Katabazi amebainisha kuwa usalama na maendeleo ni vitu vinavyoenda pamoja ili kuvidumisha ni muhimu Polisi Kata, wakaguzi na Watendaji wa Kata kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia mipaka, kanuni, taratibu na sheria zilizopo.
Vilevile Kamanda Katabazi amesisitiza maafisa wa Polisi kuzingatia maadili ya kazi zao na kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama kula rushwa, kuacha kutumia vilevi na kuwaasa kufanya tathmini kama Kata wanazosimamia zina uhalifu ili wapeleke taarifa ya maadhimio ya utekelezaji sehemu husika.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka ametoa rai kwa maafisa Polisi Kata ambao bado Kata zao zina taarifa za ulimaji bangi kujitathmini kwani swala hilo linachafua Kata hizo na utendaji kazi wao. Pia Mhe. Mayeka amegusia suala la kuwaweka watu vizuizini bila sababu kuachwa mara moja ili utulivu uliopo ndani ya Wilaya ya Kongwa uendelee.
Sambamba na hayo Mhe Mayeka ameomba Polisi Kata kupatiwa usafiri utakaowasaidia kufika kirahisi katika maeneo wanayosimamia kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu na kugusia kuwa kuna baadhi ya Kata zina Vijiji zaidi ya vitano hivyo inakuwa vigumu kiongozi wa kata kuvifikia Vijiji vyote kwa urahisi.
Hata hivyo Mhe Mayeka amevisihi vyombo vya dola vilivyopo Wilayani Kongwa ikiwemo jeshi la Polisi na jeshi la Wananchi kuacha migogogoro isiyokuwa na maana kwani wote wanategemeana katika kuleta na kudumisha amani katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa White Zuberi ameomba jeshi la Polisi kudhibiti wizi wa mifugo ili kunusuru uchumi wa wananchi wanaojihusisha na ufugaji na kukomesha matumizi ya dawa za kulevya na pombe kali ya gongo yanayoendelea ndani ya Wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.