Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kutatua kero zinazowakabili kwa muda mrefu Wakazi wa eneo la Kibaigwa wilaya ya Kongwa.
Miongoni mwa Kero hizo ni Tatizo la umeme usiokidhi mahitaji, miundombinu ya barabara, migogoro ya Ardhi na huduma za jamii..
Akizungumza na Wananchi katika eneo la Kibaigwa Julai 7, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliahidi kuwa serikali kupitia mamlaka zake itashughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika eneo hilo.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Aliwaasa Wananchi kuchukua Tahadhari dhidi ya Janga la ‘’Corona’’ kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na wataalamu wa Afya.
Aidha Mhe. Rais alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha wafanya biashara kufuata Sheria na kanuni zote zilizowekwa na Halmashauri pia wananchi wote kuhakikisha wanashiriki katika suala la ulinzi na usalama kwa kufichua watu wenye nia ya kuvuruga amani.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jobu Y. Ndugai (Mb) Jimbo la Kongwa, amemshukuru Mhe. Rais na serikali yake kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za kuendeshea miradi mbalimbali hususani ya Elimu, Afya, miundombinu na kadharika,katika jimbo la kongwa ikiwemo kata ya Kibaigwa.
Mheshimiwa Ndugai kupitia kwa Diwani wa kata ya Kibaigwa amewasilisha ombi la kuboreshewa huduma ya umeme kwani licha ya wakazi wengi kutounganishiwa umeme bado umeme uliopo hautoshelezi. Ombi lingine ni la kupanuliwa kwa maegesho ya Magari katika mji huo wa Kibiashara ili kuwezesha wajasiliamali wengi kufanya biashara kwa ufanisi.
Akijibu changamoto hizo, Mhe. Rais ameahidi kuzishughulikia na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwaajili ya miradi ya maendeleo. Na kuhusu kero ya maegesho ya magari ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na sekta husika pamoja na Halmashauri ya Kongwa wanaendelea na jitihada za kutatua kero hiyo. Kwa upande wa tatizo la umeme Mhe. Rais ameahidi kuwa suala hilo pia lipo ndani ya uwezo wa serikali kwani waziri mwenye dhamana atashughulikia ndani ya kipindi kifupi.
Licha ya wananchi kutoizungumzia Migogoro ya Ardhi iliyopo katika kata ya Kibaigwa, Mheshimiwa Rais ametaja kuwepo kwa migogoro ya ardhi na hivyo ameahidi kuwa Waziri au Naibu wa Wizara husika atafika kushughulikia changamoto hiyo.
Mapokezi hayo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan yalihudhuriwa na umati wa wananchi na Viongozi mbalimbali waliokuwa wamejipanga kando ya barabara akiwemo, Mhe. Spika wa Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Katibu tawala wa wilaya ya Kongwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa, kamati ya ulinzi na usalama mkoa, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kongwa, viongozi wa Chama (CCM) mkoa na wilaya na wengineo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.