Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule, amefanya ziara ya kwanza ya kikazi wilayani Kongwa tangu alipohamishiwa Mkoani Dodoma.
"Leo nimeanza ziara za kutembelea wananchi wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma kwa malengo matatu. Moja kujitambulisha, mbili kusikiliza kero na tatu kutoa Maelekezo ya Serikali " RC Senyamule.
Wakati wa ziara Mhe. Senyamule alifanya kikao cha ndani na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel na kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na wilaya na hatimaye kufanya ukaguzi wa Kituo cha Afya na mradi wa maji katika Kijiji cha Mkoka.
Kupitia ukaguzi huo Mkuu wa Mkoa alipongeza hatua iliyofikiwa, na kutoa maelekezo Kwa wasimamizi wa Kituo hicho cha Afya Mkoka kuwa ifikapo Oktoba 1, 2022 kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Akiwakilisha wananchi, Diwani wa Kata ya Mkoka Mhe. Richard F. Mwite amesema Kwa kushirikiana na kamati za ujenzi wa Kituo hicho cha Afya watahakikisha Maagizo yanatekelezwa, na wananchi wanapata huduma kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2022.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Songambele na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, Mkuu wa Mkoa amesikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia majibu ya papo Kwa papo kupitia wakuu wa Idara, Taasisi, vitengo na Mamlaka mbalimbali.
Naye katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Fatuma Mganga amewataka wananchi kuchangia bima ya Afya CHF na kusisitiza kuwa wale waliochangia bima hiyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma hasa upatikanaji wa dawa.
Ziara hii wilayani Kongwa, ni mwanzo wa ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa, katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.