Na Stephen Jackson, Kongwa.
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Kongwa Bwana. Cosmas Shauri, amewataka wananchi kufichua Vitendo vya Rushwa na Ubadhirifu wa fedha za umma vinavyoweza kufanywa na Viongozi wasiokuwa waadilifu.
Kamanda Shauri ameyasema hayo wakati akitoa semina kwa waumini wa Kanisa Katholiki, Parokia ya Hembahemba iliyopo Kata ya Njoge Wilayani Kongwa, Jimbo kuu la Dodoma muda mfupi baada ya kumalizika kwa Ibada ya Misa ya Jumapili.
Akirejea maandiko ya vitabu vya dini pamoja na mifano mbalimbali Kamanda Shauri amefafanua kuwa kupokea Rushwa ni kupofusha macho ya mwenye akili, na hivyo amewaasa waumini hao kutofumbia macho vitendo vya ubadhilifu kwani madhara yake ni kukosekana kwa huduma bora kwa wananchi.
Akiuliza swali kwa niaba ya Waumini, wa Kanisa hilo, Paroko Kitamboya alitaka kufahamu ni kwa jinsi gani mwananchi mnyonge anaweza kushughulika na watu wenye nguvu kiuchumi na Kimamlaka.
Akijibu swali Hilo Kamanda Shauri amesema, Jukumu la mwananchi ni kutoa taarifa, na TAKUKURU itafanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki huku ikihakikisha Usalama kwa upande wa mtoa Taarifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Hembahemba Bwana Onesmo Mdamu, ameeleza kuwa waumini wameyapokea vizuri mafundisho hayo na yamekuwa msingi ndani ya Maisha yao kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya mambo yenye viashiria vya rushwa katika Mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.
Ziara hiyo ya Kamanda wa TAKUKURU katika parokia ya Mtakatifu Luka Mwinjili, ni Mwaliko wa Kiongozi wa Parokia hiyo Paroko Gideoni Kitamboya.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.