Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Wizara ya kilimo imedhamiria kuwaondoa makanjanja katika sekta ya kilimo kwa kuanza kuwasajili maafisa ugani wa Serikali na wale ambao hawajaajiriwa kwa kuwaingiza kwenye mfumo ambao mkulima atakuwa nao kwenye simu kuwasiliana na afisa ugani moja kwa moja.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) alipokuwa akiongea na wananchi wa Kata ya Mtanana Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma katika uzinduzi wa kampeni ya Mali Shambani na uzinduzi wa mfumo wa huduma za ugani kiganjani (ugani kidigiti) yenye lengo la kuwatambua wakulima na kuwawezesha kupata taarifa za kilimo kupitia vyombo vya habari na mifumo ya kidigitali.
Mhe. Bashe ameeleza kuwa teknolojia hiyo itamsaidia mkulima kupitia simu yake ya mkononi kupata taarifa zote kuanzia hatua za awali za kilimo mpaka kupeleka mazao sokoni kutoka kwa afisa ugani aliyesajiliwa na kuthibitishwa.
Aidha Mhe. Bashe ameongeza kuwa taarifa njema kwa wakulima ni kwamba Serikali imeagiza vifaa vyenye thamani ya dola milioni 10 kuweka katika kitupo cha Taifa cha zana za kilimo vitakavyomuondolea mkulima adha ya kusafisha na kusawazisha mashamba.
Vilevile Mhe. Bashe ametumia jukwaa hilo kuwataarifu wakulima kuwa watakaponunua mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika Wilaya ya Kongwa utakuwa tofauti kwani watasajiliwa na kupewa kibali cha kwenda popote kuuza mazao yao.
Nae Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mhe. Job Ndugai ameunga mkono juhudi za serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kuleta mfumo huo wa kidigitali wa kuwasaidia wakulima kuwasiliana na wataalam wa kilimo na kuongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuwaondoa maafisa ugani waliokuwa hawatimizi majuku yao licha ya kulipwa mishahara mikubwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amewataka wananchi hususani vijana kutumia fursa za kilimo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.