Leo tarehe 22 Septemba semina maalumu kwa waandishi wasaidizi na waendeshaji wa vifaa vya bayometriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura imefunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Dkt Omary Nkullo katika ukumbi wa VETA na ukumbi wa shule ya Kongwa Sekondari.
Mamia ya waendeshaji vifaa vya bayometriki Pamoja na waandishi wasaidizi wamepata wasaa wa kupewa maarifa juu ya zoezi zima la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, pia wamekula kiapo kabla ya kutia Saini mikataba yao ya kazi husika, pamoja na kupatiwa elimu maalumu juu ya mambo mbalimbali yanayohusu zoezi husika.
Wataalamu mbalimbali kutoka tume huru ya uchaguzi wametoa somo la namna ya kutumia vifaa vya bayometriki Pamoja na afisa uhamiaji ambaye alitoa elimu ya uraia ili kuongeza uelewa kwa waandishi wasaidizi kumtambua raia anayestahili kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Waandishi wasaidizi pamoja na waendeshaji wa vifaa vya bayometriki wakila kiapo kutunza siri katika zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura.
Aidha akiongea na waandishi wasaidizi Pamoja na waendeshaji wa vifaa vya bayometriki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt Omary Nkullo amesisitiza uadilifu kwa wahusika katika zoezi zima Pamoja na kuhakikisha wananchi wote watakaojitokeza katika zoezi hilo wanapatiwa ushirikiano ipasavyo ili zoezi hilo lifanikiwe kwa asilimia mia moja. Pia waendeshaji vifaa vya bayometriki wameaswa kuwa waangalifu na vifaa kuhakikisha wanavitunza katika siku zote za zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura kwani ni vifaa vya gharama kubwa na vinahitajika kuwa katika ubora huo huo waliovipokea kipindi watakapovirudisha zoezi litakapofikia tamati.
waendeshaji vifaa vya bayometriki wakipata mafunzo katika semina elekezi.
Semina hiyo elekezi kwa waandishi wasaidizi Pamoja na waendeshaji vifaa vya bayometriki itafanyika kwa siku mbili na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litaanza wilayani Kongwa siku ya tarehe 25 Septemba na kufanyika hadi ifikapo tarehe 1 Oktoba mwaka huu.
Imeandaliwa na
Mbonea Masha
Afisa Habari Halmashauri ya wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.