Katibu tawala wilaya ya Kongwa Bi Sozi Ngate amepongeza kanisa Katoliki la Mtakatifu Fransisco wa Asiz Kongwa kwa juhudi zake za kushirikiana na Serikali na kuongeza kuwa Serikali inatambua mchango wake katika kuleta maendeleo.
Bi Sozi ameyasema hayo kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Mayeka Simon Mayeka katika uzinduzi wa albam yenye nyimbo Saba za Injili ya kwaya ya Mtakatifu Sesilia Kanisa Katoliki la Mtakatifu Fransisco wa Asiz Kongwa iliyoanzishwa mwaka 1973 ambapo ameipongeza kwaya hiyo kwa hatua waliyofikia ya kurekodi video kuwa ni uamuzi mzuri.
Aidha Bi Sozi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wa Serikali wanasisitiza ushirikiano kati ya taasisi za dini na Serikali kwa ustawi wa Taifa kwani taasisi za dini licha ya kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia miradi ya maendeleo lakini pia zimekuwa zikisaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Vilevile Bi Sozi ameomba Viongozi wa Taasisi za dini kudumisha umoja na mshikamano na pia kumuombea Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kazi kubwa anayozofanya lakini pia kuwaombea viongozi na Taifa kwa ujumla na Taifa kuwa na amani na utulivu wa kutosha.
Bi Sozi ameweka wazi kuwa jamii imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili na matukio mbalimbali lakini anawapongeza Viongozi wa dini Kwa mchango wao wa kukuza imani na kufundisha maadili kwa waumini wao na kusaidia kupunguza matukio hayo katika jamii.
Akijibu changamoto za kwaya ya Mtakatifu Sesilia Kongwa zilizosomwa katika risala maalum na Mwenyekiti msaidizi wa kwaya hiyo Bw John Charles, Bi Sozi ameeleza kuwa Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kongwa itachangia kulingana na itakavyobarikiwa hadi kumaliza changamoto hizo changamoto mojawapo ikiwemo ni ukosefu wa kinanda.
Mbali na hayo katika hafla hiyo ya uzinduzi wa albam hiyo iliyohudhuriwa na viongozi na watu mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Kongwa bi Sozi ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuhakikisha wanapiga kura siku ya tarehe 27 Novemba kuwachagua viongozi wao wa Mitaa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.