Na Stephen Jackson, Kongwa
Serikali wilayani Kongwa, imepanga kuunda kamati maalumu itakayohusika na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa.
Kauli ya kuundwa kwa kamati hiyo maalumu imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, wakati akizungumza na wajumbe wa kamati kuu ya mbio maalumu za mwenge wa uhuru 2021 wilayani hapa, katika ukumbiwa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa wakati wa kikao cha Tathmini ya shughuli za Mapokezi ya Mwenge kwa mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Mhe. Mwema, Kamati hiyo itakuwa ikifanya ufuatiliaji wa karibu kwa miradi yote inayotekelezwa wilayani hapa, ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohusu Miradi yote inayoendelea.
Kufuatia mpango huo, Mhe. Mwema amewaagiza wakuu wa Idara na vitengo ndani ya Halmashauri kuwa na ratiba ya kutembelea miradi yote ya maendeleo na kuitolea taarifa kila mwezi ikiwa ni pamoja na kuwajulisha wananchi. Katika taarifa zao, wakuu wa Idara, watapaswa kueleza changamoto walizozibaini kwa kila mradi na kupendekeza njia au mbinu bora za utatuzi.
Kuhusu Miradi ya uwekezaji wa Madini mkuu wa Wilaya amewataka wawekezaji kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji wakati wa kufanya makubaliano ya tozo ili kuepuka tabia ya utoroshaji wa madini kwa kuwa kitendo hicho kinakwamisha maendeleo. Ameongeza kuwa wakati wa makubaliano baina ya viongozi wa vijiji na wawekezaji ni lazima Mwanasheria wa Halmashauri ashirikishwe kikamilifu.
Ilikudhibiti tatizo la utoroshaji wa madini unaofanywa na baadhi ya watu wasio na uzalendo, Mhe. Mwema ameahidi kufanya kikao na wadau wa Madini wilayani Kongwa kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wilaya iweze kukusanya mapato kutokana na uwepo wa Madini wilayani Kongwa.
Wakati huo huo Mhe. Mwema ametangaza kampeni ya kufyatua Matofali laki moja kwa kila kijiji ili kuwezesha ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya elimu na Afya. Mhe. Mwema alitoa maelekezo hayo kwa wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake asubuhi ya trehe 11 Agosti 2021, na baadaaye kwa wajumbe wa kikao cha tahmini ya mapokezi ya Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2021.
Wajumbe wa kamati mbalimbali za mapokezi ya mwenge wa uhuru walikutana tarehe 11 Agosti 2021 kutathmini shughuli mbalimbali zilizofanyika, ikiwemo uchambuzi wa taarifa za miradi, pamoja na mapato na matumizi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.