Na Stephen Jackson, KDC
Viongozi wa dini wameishauri serikali kutafuta njia mbadala ya kuwasaidia watu wenye ulemavu badala ya kuwakopesha fedha kwa kuwa wengi wao hawana elimu ujasiriamali.
Ushauri huo umetolewa Mei 4, 2023 na Mchungaji Kanoni Agripa Ndatila, Mkuu wa chuo cha Theolojia cha Mt. Philip kilichopo wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, wakati wa mkutano wa kimataifa wa wakuu wa vyuo vya theolojia uliofanyika chuoni hapo ukihusisha mataifa matano.
Akifafanua hoja hiyo, Kanoni Ndatila alisema chuo hicho kinaendesha programu maalumu ya kutoa elimu juu ya namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa miaka nane sasa, hivyo wamebaini kuwa njia bora ya kuwasaidia ni kuwafundisha ujuzi mbalimbali ili waweze kujitegemea.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuhitimishwa kwa mkutano, Mchungaji Dkt. Daniel N.Karanja kutoka kanisa la Episcopal Marekani ameitaka jamii kubadili mtazamo kuhusu watu wenye ulemavu kwa kutambua umuhimu wao na kwamba jamii inahitaji mchango wao.
Kwa upande wake msemaji mkuu katika Mkutano huo Mchungaji Dkt. Emily Awino Onyango mkufunzi katika chuo kikuu cha Mt. Paul nchini Kenya aliwataka viongozi wa dini kutafsiri vizuri maandiko ili kuwezesha watu wenye ulemavu kupata ahueni ya Maisha. Katika wasilisho lake alisema endapo viongozi wa dini watatimiza wajibu huo, itasaidia kupunguza changamoto katika masuala mengine ya kijamii ikiwemo ukatili wa kijinsia.
Akitoa maoni yake Kanoni Hilda Kabia Mkuu wa chuo cha Theolojia Msalato alisisitiza kuwepo na miundombinu wezeshi katika kila taasisi ili kupunguza adha kwa watu wenye ulemavu.
Naye Mratibu wa Mpango wa walemavu Mchungaji Naftaly Zabroni kutoka chuo cha Mt. Philip ameitaka jamii kuwajali walemavu ikiwa ni pamoja na kuwatembelea na kuwasaidia kwa hali na mali.
Kufuatia maudhui hayo, mchungaji Kanoni Edward Martin Komba Mkuu wa Chuo cha Mt.Marks kilichopo jijini Dar es Salaam akawashauri viongozi wa dini kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali katika jitihada za kuboresha Maisha ya watu katika jamii.
Awali Mkurugenzi wa programu ya walemavu nchini Bi. Wendy Broadbent raia wa Amerika alisema Tanzania inazo sera na sheria nzuri zinazolinda watu wenye ulemavu
Viongozi wengine wa mataifa ya Afrika walioshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja na Mchungaji Kahwa Njonjo (DRC), Mchungaji Jesee Mutugi (Kenya) na Dkt. Pascal Bigirimana kutoka Burundi.
Mpango huo umefadhiliwa na Ofisi ya Global partnership ya nchini Malekani na unasimamiwa na wachungaji David Copley (USA) na Dkt. Daniel N. Karanja (Afrika)
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.