Viongozi, wananchi na wadau mbalimbali wametakiwa kushirikiana Ili kufanikisha ujenzi wa Madarasa 70 kupitia fedha shilingi bilioni Moja na milioni mianne kutoka serikali kuu.
Hayo yamebainika katika kikao Cha tathmini ya ujenzi wa Madarasa hayo, kilichofanyika Oktoba 9, 2022 katika ukumbi wa VETA Kongwa ambapo Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Mwema Emmanuel alikuwa mgeni Rasmi.
Aidha Mhe. Mwema amewataka watendaji wa vijiji na kata kuwashirikisha wananchi na wataalam katika kila hatua za ujenzi ili kuepuka malalamiko na changamoto za kujenga majengo chini ya kiwango.
Akizungumza wakati wa kikao, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila, amewataka walimu wakuu kushirikiana na kamati za ujenzi kufanya Kazi ili ujenzi ufanyike kwa wakati uliopangwa.
Akiunga mkono ushirikiano huo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wilaya ya Kongwa Ndugu Fortunatus Mabula ametaja ushirikiano kama mbinu muhimu ya Kufanikisha ujenzi. Amesema kuwa ushirikishwaji wa pamoja wa taarifa utachochea ujenzi bora na wa haraka wa madarasa hayo.
Naye Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ndugu Musa Abdi amepongeza jitihada za serekali za kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa Madarasa.
Akitoa rai katika hafla hiyo mshauri wa jeshi la akiba wilaya Meja Henry Mwakipesile amesema msingi mkubwa ni uzalendo kwani madarasa hayo ni kwaajili ya watoto wetu na lazima hatua kali zichukuliwe kuhakikisha ujenzi unakamilika.
Naye Mkuu wa Gereza la Kongwa SP Tekla Ngilangwa, ameiomba halmashauri kuendelea kuiamini ofisi yake kwa kuwapa nafasi wafungwa kujenga madarasa hayo.
Serikali imetoka Tsh 1,400,000,000.00 kwaajili ya ujenzi wa madarasa 70 ya shule za Sekondari wilayani Kongwa ambapo kila darasa litagharimu Tsh 20,000,000.00 hii itasaidia kutatua changamoto za miundombinu ya elimu, ambapo madarasa hayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 30 mwaka 2022
Kwa Mujibu wa agizo la Mheshimiwa Mwema, ujenzi huo unatakiwa kuanza ndani ya wiki moja kuanzia sasa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.