Na Mwandishi Wetu, Kongwa DC
Shule ya Msingi Kongwa imepokea msaada wa samani za shule wenye thamani ya shilingi 6,520,000/= kutoka kwa wadau wa elimu wa kanisa la kiinjili la kilutheri la Ujerumani Februari 19, 2024.
Msaada huo umetolewa na Familia ya Bwana Joachim Grtzyk raia wa ujerumani ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa kanisa la ELC nchini Ujerumani na Tanzania alipotembelea kanisa rafiki la KKKT Kongwa na hakuunganishwa na shule hiyo.
Joachim alinukuliwa akisema, yeye na mke wake bi. Elsbeth walianza urafiki na shule hiyo tangu mwaka 1992 na wamekuwa wakiguswa na changamoto za kielimu kwa shule hiyo, ikiwemo wanafunzi kukaa chini, hivyo wamekuwa wakisaidia kwa kiasi fulani licha ya kuwa hawana uwezo mkubwa.
Akiwasilisha taatifa katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo, Beatrice Mbijima, Mwalimu mkuu msaidizi wa wa shule hiyo alisema, jumla ya madawati 60, viti 21, meza 5, na kiti kimoja kwa ajili ya Mwalimu mkuu vimepatikana kutokana na mchango wa wahisani hao wa shilingi 6,520,000/= zilizopokelewa kupitia Dinari ya Mpwapwa.
Taarifa ya shule inabainisha kuwa, msaada uliotolewa utasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kukaa chini na kuondoa dosari ya upungufu wa viti na meza za walimu.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri Dkt. Omary Nkullo, Afisa utumishi Bwana Evodius Rugainunura Rugeiyamu aliwashukuru wadau hao kwa uamuzi wao wa kuisaidia serikali kutatua changamoto katika utoaji wa huduma za jamii na kwamba serikali inathamini sana jitihada hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Shule, Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bwana Gabriel Wilson Mgohachi alitoa shukrani za dhati kwa shule hiyo na kuwaomba wahisani hao wasichoke kuisaidia shule, kwani bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na uongozi mzima wa shule, Walimu na kamati ya shule, Mgeni rasmu akiwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri aliyewakilishwa na ndugu Evodius Rugeiyamu aliyeongozana na Mwakilishi wa Afisa Elimu Msingi mwalimu Jane Lutego huku wadau hao wakiambatana na viongozi wa kanisa la KKKT Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.