Na Bernadetha Mwakilabi, Kongwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Kongwa imetoa elimu kwa Askari wa Jeshi la Polisi Wilayani Kongwa.
Semina hiyo imefanyika tarehe 25 Septemba katika ukumbi wa Polisi Jamii Kongwa ambapo Askari hao wameweza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na utendaji wa kazi wa Taasisi hiyo pamoja na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 rejeo la mwaka 2022.
Akitoa elimu hiyo Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Cosmas Shauri amesema kuwa majukumu ya Taasisi hiyo kwa ufupi ni Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambapo Taasisi hiyo inatekeleza jukumu la kuzuia Rushwa kwa kushirikisha Umma katika mapambano dhidi ya Rushwa hivyo jamii ikielewa vyema dhana ya mapambano dhidi ya rushwa basi kazi ya kuzuia rushwa itakuwa rahisi. Wananchi wakielewa vema wataweza kufuatilia miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kutoa taarifa TAKUKURU mara wanapobaini uwepo wa vitendo vya rushwa, pia wananchi wakielewa ubaya wa rushwa itakuwa rahisi kukataa kujihusisha na vitendo hivyo.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa alieleza kuwa ofisi inazuia rushwa kwa kufanya tafiti na kupitia mifumo ya utendaji kazi ya Taasisi za Serikali, zisizo za kiserikali pamoja na mashirika ya umma ili kubaini mianya ya rushwa katika mifumo hiyo na kutoa mapendekezo kwa taasisi na mashirika husika jinsi ya kuziba mianya hiyo.
Akielezea kuhusiana na Kupambana na rushwa, Bw. Shauri alieleza kwamba baada ya kuwa vitendo vya rushwa vilishafanyika basi Taasisi hiyo inakuwa haina budi kupambana ambapo kunahusisha kufanya uchunguzi wa vitendo vya rushwa na kuwafikisha Mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Moja ya makosa yaliyofafanuliwa ni pamoja na kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na sheria lililopo chini ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa sura ya 329 rejeo la mwaka 2022, imeelezwa kwamba ni kosa kwa mtu yoyote mwenye mamlaka ya kutoa huduma fulani kuomba kitu chochote chenye thamani (fedha au mali) ili aweze kutoa huduma hiyo, au aache kutekeleza majukumu yake ya kikazi na kwamba kile kitu kinachotolewa kwa mtu huyo ili atimize au asitimize wajibu wake ndicho kinajulikana kuwa ni rushwa.
Aidha Bw Shauri alieleza kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ni kosa kwa mtu yoyote kutoa rushwa kwa mtu yoyote mwenye mamlaka ya kutekeleza jukumu fulani ili atekekeze au asitekeleze jukumu hilo.
Kosa lingine ambalo alifafanua ni kosa linalotokana na kifungu cha 22 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 rejeo 2022 ambacho kinakataza matumizi ya nyaraka zenye maelezo ya uwongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri, akifafanua kosa hili alitolea mfano wa mtumishi ambaye anatumwa kwenda safari ya kikazi na mwajiri wake ambapo anakuwa amepangiwa kwenda kufanya kazi hiyo kwa muda wa siku saba lakini kazi hiyo ikafanyika kwa siku tatu, na yeye akaendelea kuomba kiasi cha fedha ya siku saba nakuwasilisha maombi hayo kwa mwajiri wake, hiyo hati ya malipo aliyoomba malipo ya siku saba itakuwa ni nyaraka yenye maelezo ya uwongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake.
Akifafanua kuhusiana na kifungu cha 29 cha sheria hiyo, Bw. Shauri anasema ni kosa kwa mtu yoyote kuchepusha mali za umma. ametolea mfano wa mfanyakazi kuhamisha mali ya ofisi na kwenda kuitumia kwa maslahi yake binafsi, mfano wa mali hiyo kuwa yaweza kuwa vifaa vya ofisi, magari, pikipiki na vaifaa vingine vinavyofanana na hivyo.
Kosa lingine linatoka kifungu (25) ambapo kifungu hiki kinahusiana na rushwa ya ngono kinachoeleza kuwa ni kosa kwa mtu yoyote mwenye mamlaka ya kufanya jambo fulani au kutekeleza wajibu fulani kushawishi au kuomba ngono ili aweze kutekeleza jambo hilo ambalo linahusiana na majukumu yake ya kila siku.
Vilevile Bw. Shauri amefafanua kuwa kifungu (27) cha Sheria hiyo kinahusu mtumishi wa Umma kuishi maisha ambayo hayalingani na kipato chake aidha kinahusu mtumishi wa umma kumiliki mali ambazo hazilingani na kipato chake.
Amefafanua kwamba iwapo uchunguzi wa awali utabainisha kwamba mtumishi fulani anamiliki mali zisizolingana na kipato chake, ofisi ya TAKUKURU itampatia mtumishi huyo Ilani ya kujieleza ambapo ataeleza mali alizonazo na jinsi alivyozipata na iwapo atashindwa kueleza kuwa ni jinsi gani amezipata mali hizo basi sheria itazitambua mali hizo kuwa zimepatikana kwa njia ya rushwa hivyo mtuhumiwa huyo akitiwa hatiani mahakamani mali hizo zitaweza kutaifishwa.
Aidha akielezea umuhimu wa Jeshi la Polisi kupata elimu ya rushwa amesema elimu hii ni kwa ajili ya Askari wa Jeshi la Polisi kutojihususha na vitendo vya rushwa lakini pia ni kwa ajili ya wao kutoa ushirikiano wanapokutana na vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa katika ofisi ya TAKUKURU ili kufanyia kazi vitendo hivyo vya rushwa.
Ma-afisa wa jeshi la polisi wakisikiliza kwa makini mafunzo katika semina elekezi.
Nae Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Severine Kisuda amesema kuwa asilimia kubwa ya maeneo yanayolalamikiwa ni wakati wa upelelezi wa makosa na makosa ya usalama barabarani ambapo amewasihi Jeshi la polisi kubadilika kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu kuwasaidia raia kupata haki zao kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa polisi Wilaya ya Kongwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Omary Mwanyika ameshukuru TAKUKURU kwa elimu ya Rushwa waliyoitoa na kuwataka Askari kufuata utaratibu wa kazi, aidha ameomba Takukuru kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu kwa Askari ili wajue makosa ya rushwa na namna ya kuepukana nayo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.