Na Bernadetha Mwakilabi, Kongwa
Moja ya wajibu wa viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya rushwa kwanza kabisa wao wenyewe wasijihusishe na vitendo vya rushwa katika kipindi cha Uchaguzi na mahali pengine popote kwani wao kama binadamu wanaweza kukutana na vitendo hivyo na wakashiriki kwa kujua au kutokujua. Hayo yameainishwa katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU walipokutana na viongozi wa dini katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mapema wiki hii.
Akiongea na viongozi wa dini, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Cosmas Shauri amesema Rushwa ni dhambi kwa mujibu wa maandiko matakatifu hivyo viongozi wa dini wana wajibu wa kushughulikia rushwa kwa waumini wao kama wanavyoshughulikia dhambi nyingine, ameongeza pia kwamba viongozi wa dini wana kundi kubwa linalotegemea huduma ya kiroho hivyo ni vyema wakatumia nafasi hiyo kuwafundisha na kuwasisitiza madhara ya kuwachagua viongozi wala rushwa.
Aidha Bw. Shauri amewaasa viongozi hao wa dini wasipokee zawadi toka kwa wagombea ili wawaruhusu kutumia nyumba za ibada kufanya kampeni.
Bw Shauri ameelezea kuwa michakato ya Uchaguzi na uteuzi wa wagombea katika vyama vya siasa imekuwa hatarini kwa kugubikwa na vitendo vya rushwa na udanganyifu, ambapo wagombea wamekuwa wakiwapa wanachama fedha ili waweze kuwachagua na baadhi wamekuwa wakiwanunulia, chakula, pombe na hata kuwasafirisha kwenda kupiga kura.
Bw Shauri ameendelea kwa kuelezea kuwa Rushwa imetajwa katika maandiko matakatifu katika Qur'aani tukufu sura ya 2 aya ya 188 ambayo inasema "wala msiliane mali zenu kwa ubatili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua". Pia katika upokezi utokanao na Swahaba Ibnu Umar amesema "mtoa rushwa na mpokea rushwa Makazi yao ni motoni"
Pia katika Biblia Takatifu Injili ya Luka 3:14 Wakati Yohana Mbatizaji akiwaasa watu watubu, "askari nao wakamwuliza wakisemea sisi nasi tufanye nini? Akawaambia msidhulumu mtu wala msishtaki kwa uwongo tena mtosheke na mshahara wenu". Pia Injili ya Mathayo 28:12-13 "wakakusanyika pamoja na wazee wakafanya shauri wakawapa askari fedha nyingi wakisema semeni ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku wakamwiba tulipokuwa tumelala".
Bw. Shauri, Pia amefafanua madhara ya rushwa katika Uchaguzi kuwa ni kuondoa uhuru wa mpiga kura, pale wagombea wenye vipaji na uwezo wa kuwasilisha, kushindwa kushiriki kugombea katika Uchaguzi kwa kukosa uwezo wa kifedha, hii hupelekea rushwa katika Uchaguzi kuzuia wananchi kuwapigia kura viongozi wanaowataka.
Ameongeza kuwa rushwa huharibu dhana nzima ya uwakilishi kwa kuwa wanaochaguliwa hawana ridhaa kamili ya mpiga kura lakini pia viongozi waliochaguliwa kwa njia ya rushwa hawawezi kusimamia mapambano dhidi ya rushwa wakiwa madarakani na usimamizi wa shughuli za maendeleo hukwama kutokana na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Bw. Shauri amehitimisha kwa kusema kuwa madhara ya rushwa katika jamii huikumba jamii yote ambayo viongozi hao wapo, hivyo nao ni waathirika wa madhara hayo lakini wakiungana wote kwa umoja wao wataweza kupunguza rushwa kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu.
Kwa upande wake Afisa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Severine Kisuda amesema Uchaguzi ni mchakato ambao watu wa eneo la Uchaguzi wanatumia kutafakari mustakabali wa maendeleo yao katika eneo na lengo lake hasa ni kupata viongozi waadilifu waaminifu watakaojali maslahi ya jamii kwa kuhakikisha wanawaongoza wananchi kuweka mipango ya kuendeleza eneo lao na kulisimamia.
Afisa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU Bw. Severine Kisuda akitoa elimu kwa viongozi wa dini.
Kisuda amesema baadhi ya wanasiasa hupenda kutumia rushwa ili kuingia madarakani kwa kuwarubuni wapiga Kura ili wawachague hivyo wananchi watambue umuhimu wa kushiriki Uchaguzi kwa ustawi wa maendeleo yao na Taifa hivyo waache kuchagua viongozi wanaogawa zawadi fedha nguo chakula n.k.
Amewasihi viongozi wa dini kutoa elimu kwa wananchi kushiriki Uchaguzi bila kujihusisha na vitendo vya rushwa kuepuka vurugu machafuko vita mauaji na ghasia, na kuwaeleza kuwa wanaweza kutoa taarifa kwa kufika ofisi za TAKUKUKURU au kupiga simu ya Bure namba 113.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wengine wa Dini Shekh Iddi Binde wa msikiti Masjid Qubaa amesema wamepokea mafundisho hayo na kuahidi kushirikisha waumini katika kila ibada wanazofanya kuanzia Sasa ili watambue vitendo na viashiria vya rushwa hususani katika kipindi hiki cha Uchaguzi ili wawatambue na wachague viongozi watakaowaongoza vizuri na kuwaletea maendeleo.
Kikao hiki ni muendelezo wa vikao ambavyo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa imeendelea kufanya na makundi mbalimbali yenye ushawishi katika jamii ili kuelimisha na kutoa elimu ya rushwa kipindi ambacho nchi yetu inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa. TAKUKURU imeendelea kusambaza ujumbe kwa kutumia kauli mbiu yake isemayo, Kila mmoja wetu akisema , “nazuia rushwa katika uchaguzi ili nipate viongozi waadilifu na watakaotekeleza kwa ufanisi mipango ya maendeleo.” Tutakuwa tumemshinda adui rushwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.