Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma imewajengea uwezo wafanyabiashara wa Mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa kuhusu mabadiliko ya Sheria za kodi Kwa lengo la kuondoa mkanganyiko wakati wa utekelezaji wa Sheria hizo.
Akitoa semina Kwa wafanyabiashara hao, Afisa Msimamizi kodi mwandamizi ndugu Philipo Eliamini ametaja mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika kwenye Sheria, na taratibu zinazotumika kufanya makadirio, na aina za kodi zinazopaswa kulipwa.
Aidha bwana Eliamini ametilia mkazo umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu za biashara ikiwemo matumizi "EFD". Sanjali na hayo amewataka wafanyabiashara kusajili maghala na stoo wanazomiliki, na kuhakikisha wanadai risiti kila wanaponunua na kuuza bidhaa.
Aidha Ndugu Eliamini ameongeza kuwa, endapo mfanyabiashara atanyimwa risiti Kwa bidhaa alizonunua atapaswa kutoa taarifa kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato zilizo karibu naye ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Kwa upande wake Afisa biashara wa Halmashauri ndugu Yonaza Mchome amewataka wafanya biashara kutoa taarifa Ofisi ya biashara pindi wanapofunga biashara zao badala ya ilivyozoeleka kwamba mfanyabiashara hutoa taarifa ya kusitisha biashara yake kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato pekee.
"Ni vizuri unapofunga biashara, ni vizuri tukapata taarifa ofisi yetu ya biashara lakini pia ukatoa taarifa kwa wenzetu wa TRA". Alisema Ndugu Mchome.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Tech import & Export LTD. ya Kibaigwa inayojihusisha na usafirishaji wa nafaka Bi. Gath Marwa, amesema kwamba binafsi semina hiyo imemwezesha kujua aina za Kodi anazopaswa kulipa tofauti na alivyokuwa akijua awali na amewashauri wafanyabiashara kuacha kukwepa kodi, kwani kulipa kodi ni moja ya uzalendo.
Kwa mujibu wa miongozo ya TRA wafanyabiashara ambao mauzo yao ni chini ya milioni 14 kwa mwaka, ndio pekee wanaoruhusiwa kutumia vitabu vya risiti vinavyoonesha Namba ya mlipa kodi (TIN) pamoja na taarifa zingine kuhusiana na biashara yake, na yeyote ambaye biashara yake inazidi kiwango hicho anapaswa kutumia Mashine ya kielektroniki ya EFD.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo Cha Kodi Kibaigwa ndugu Ezekiel Shekiyandumi amewakumbusha wafanyabiashara kujenga tabia ya kuandika barua za taarifa ya kusitisha biashara zao pindi wanaposhindwa kuendelea nazo ili kuruhusu maafisa wa kodi kufanyia kazi taarifa hizo kwenye mfumo wa kodi.
Akifunga semina hiyo Diwani wa Kata ya Kibaigwa Mhe. Chande Mrisho amesema, karibu 30% ya Mapato ya Halmashauri hutoka kwenye Mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa, hivyo amewahakikishia wawezeshaji wa semina hiyo kuwa yote waliyoelekeza watayafanyiwa kazi na kuitaka Mamlaka ya Mapato kuendelea kutumia busara ili kujenga mahusiano mema na wafanyabiashara.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.