Rai imetolewa kwa jamii kutofumbia macho matukio ya kikatili yanayotokea katika jamii ili kokomesha vitendo hivyo.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kongwa katika maadhimisho ya Siku ya ya familia Duniani yaliyofanyika katika Kata ya Makawa ambapo ameeleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi kumekuwa na matukio 6 ya ukatili ambapo kati yake kesi 3 zipo mahakamani na kesi 3 zinaendelea kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi.
Aidha Bi Sozi Ngate amewasihi wazazi kuzidisha ulinzi na usalama kwa Watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0-8, kuacha maneno ya maudhi, vipigo, pamoja na kuwapatia watoto elimu, huduma za Afya, lishe bora ili kuwaepusha watoto na changamoto mbalimbali.
Vilevile amefafanua kuwa baadhi ya sababu ikiwemo mafarakano na migogoro katika familia zimepelekea malezi duni kwa watoto pamoja na uangalizi hafifu hivyo kupelekea watoto kujilinda pamoja na kujitafutia mahitaji yao wenyewe, changamoto inayosababisha kuwa na kundi kubwa la watoto wa mitaani na kupelekea kundi hili kujiingiza katika vitendo visivyo na maadili katika maisha yao.
Naye Afisa maendeleo ya jamii Bi. Faraja Kasuwi ametaja kauli mbiu ya maadhimisho hayo 2025 kuwa ni "Mtoto ni malezi; msingi wa familia bora kwa Taifa imara" inayolenga kuwakumbusha wazazi na walezi jukumu lao la msingi kuwa ni malezi ya watoto ili kujenga msingi imara wa familia na hatimaye kuwa na Taifa imara la baadae.
Bi Kasuwi ameongeza kuwa wazazi Wana wajibu wa kuwalea watoto ili kujenga Taifa lenye watoto wanaojitambua, kujithamini na wenye maadili mema, na kuongeza kuwa wazazi wana wajibu wa kudumisha amani na upendo katika familia zao ili kuepusha migogogoro isiyo ya lazima inayoweza kusababisha watoto kukosa huduma muhimu za malezi na makuzi.
Akiongea kwa niaba ya wazazi Bi Herieth Mkopi wa kijiji cha Makawa amewasihi wazazi wengine kuzingatia suala la kuwapeleka watoto kliniki kupata chanjo, kupima uzito na Kujua kama wana maradhi yoyote yanayowasumbua ili wapatiwe huduma za kitabibu mapema.
Nae Yakobo Elias mwanafunzi wa shule ya Sekondari Makawa amezitaja haki za watoto kuwa ni pamoja na kuishi, kulindwa, kusomeshwa, kusikilizwa na kupatiwa mavazi, makazi na chakula.
Madhimisho hayo yalichagizwa na midahalo mbalimbali ikiwemo haki na usalama wa mtoto, malezi na makuzi, elimu ya kupinga ukatili, elimu ya lishe na uzazi salama, elimu ya Msaada wa kisheria na maelezo ya nishati Safi ya kupikia.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.