Tarehe 27 Novemba 2024 ni tarehe muhimu iliyosubiriwa kwa hamu kwani tukio muhimu la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linafanyika. Wananchi wanapata fursa ya kuchagua viongozi wao watakaowahudumia kwa miaka mitano ijayo
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kupiga kura Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S. Mayeka ameeleza kuwa, "Wananchi ni wajibu wetu kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ili kuchagua viongozi watakaotuletea maendeleo." Mhe. Mayeka S. Mayeka ameyasema hayo katika kituo cha kupigia kura kilichopo Kongwa shule ya Msingi ambapo alipata wasaa wa kumchagua mwenyekiti wake wa Kitongoji.
Aidha msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kongwa Dkt. Omary Nkullo baada ya kupiga kura, amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwani zoezi ni la dakika chache na sababu siku husika ni siku ya mapumziko, basi wasikae nyumbani na kuacha kujitokeza kwa ajili ya kutimiza haki yao ya kikatiba. Akielezea namna zoezi linavyoendelea Dkt. Nkullo amesema, "Vituo vyote kwa kupigia kura viko wazi na Wananchi wanaendelea kujitokeza kushiriki zoezi la kupiga kura.
Kwa upande wake Katibu tawala wa Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate ameeleza kufurahishwa na wepesi wa zoezi hilo na kuonyesha kupendezwa na wananchi kutoa kipaumbele kwa wazee na watu wenye ulemavu kuweza kupiga kura kwanza ili wasikae kwenye foleni ndefu. Akizungumza na wananchi Bi. Sozi alisema, "Nimeshiriki kiamilifu zoezi la kumchagua kiongozi atakayeniletea maendeleo, unasubiri nini?"
Mbunge wa Jimbo la Kongwa na spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai pia ameshiriki zoezi la kupiga kura na ameeleza umuhimu wa wananchi kutimiza haki yao ya kikatiba akitanabaisha kuwa maendeleo yanaanza na viongozi wa serikali za mitaa, ambao ndio wanaopeleka kero na hoja za wananchi Kwenda ngazi za juu za uongozi wa Serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa. Mhe. White Zuberi baada ya kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura alisema kuwa, "Mwenyekiti wa Kitongoji ni kiongozi wa karibu Sana na Wananchi ambaye ni rahisi kujua kero za wananchi na kuzipeleka mbele kwenye ngazi za juu za uongozi wa Serikali Ili kupatiwa utatuzi, hivyo ni muhimu Sana kushiriki uchaguzi Ili kuchagua kiongozi ambaye ataleta maendeleo."
Wananchi ambao wanaendelea kujitokeza katika vituo mbalimbali vya kupigia kura wanafurahishwa na muda mchache wanaotumia kupiga kura na kuondoka Kwenda majumbani kwao huku wengi wakifurahi kuchagua viongozi wanaowataka wawaongoze miaka mitano ijayo.
Mwananchi Shiriki zoezi la kupiga kura kuchagua kiongozi wa kukuletea maendeleo. Kura Yako ni muhimu.
Imeandaliwa na,
Mbonea Masha
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (W) Kongwa
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.