Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Omary Nkullo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe amewaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa lishe bora ni muhimu kwa Jamii, kwani lishe bora hupunguza Magonjwa ikiwemo Utapiamlo kwa Watoto.
Jamii inapaswa kutambua kwamba lishe bora ni muhimu kwa Watoto na inasaidia mtoto kuwa na Afya njema kimwili na kiakili, hivyo ni vema Jamii kutumia lishe bora kwa kuzingatia makundi ya vyakula, ikiwemo kundi la wanga, protini na vitamini. Aidha, amesisitiza kila mzazi kuhakikisha anachangia lishe mashuleni, kwani kwa kufanya hivyo wanafunzi wanaopata lishe bora hata uelewa wao pia utakuwa mzuri kuliko wasio na lishe bora.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Magreth Kagashe ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo ya Lishe amesema, kwa sasa hali ya lishe Wilayani humo ni ya wastani, na kwa upande wa Tatizo la Utapiamlo kwa watoto hususani wa chini ya miaka mitano lipo.
Aidha, Dkt. Kagashe amesema, kumekuwa na Changamoto kubwa ya kutofautiana kwa Takwimu za Wilaya kuhusiana hali ya Utapiamlo na Taasisi Tofauti zinazofanya tafiti za Utapiamlo; Hali inayoleta Mkanganyiko kwa Jamii katika kutambua ukubwa wa Tatizo Wilayani humo.
Dkt. Kagashe amesema kuwa, kwa sasa Timu zilizoundwa kufanya Kazi ya kutambua ukubwa wa Tatizo hilo ikishirikisha wahudumu wa Afya 217 katika vijiji 87 vya Wilaya hiyo wapo katika hatua za mwisho kukamilisha zoezi hilo, hivyo Wilaya itatoa Takwimu halisi za Utapiamlo kwa mwaka 2017/2018 Ifikapo July 15.
Kufuatia mkanganyiko huo Wajumbe wa Baraza hilo wameazimia Taasisi zote zinazofanya Tafiti za lishe Ndani ya wilaya hiyo washirikishwe katika vikao vya Kamati hiyo ili nao waishirikishe Kamati vigezo wanavyotumia katika Tafiti wanazofanya ili kuondokana na mkanganyiko huo wa Takwimu za Hali ya Utapiamlo.
Pia, Dkt. Kagashe amesema Changamoto kubwa ya ukosefu wa lishe bora, ni Jamii kutokuwa na elimu ya Lishe bora, na kupelekea Jamii kushindwa kuhifadhi mazao hususani mazao ya karanga, alizeti ambayo ni mazao muhimu katika lishe bora na kupelekea Jamii kutumia vyakula vya aina moja.
Kwa msisitizo amesema "Unakuta uji wa mtoto umechanganywa mahindi, mtama, mchele, uwele, ulezi ambazo ni nafaka tupu, wazazi wanakuwa wameuza karanga zote, kama ana ng'ombe maziwa yote anauza, mayai yote ya kuku yanauzwa, na kupelekea Mtoto anakuwa anakula chakula aina moja ambapo ni hatari kwa Afya".
Mwishowe, Dkt. Kagashe amesisitiza kwamba Jamii iondokane na uuzaji wa vyakula vyote na badala yake iwe utamaduni wa kutunza mazao ya chakula ya aina mbalimbali kama karanga, nafaka, mazao aina za kunde ili kuwawezesha kujiepusha na Tatizo la Ukosefu wa Lishe Bora.
Sambamba na hayo Kamati imeshauri Muongozo wa Kamati ya Lishe ulioandikwa kwa Lugha ya Kiingereza utafsiriwe kwa Lugha ya Kiswahili kwani Lugha ya Kiingereza ni Changamoto kubwa katika Jamii ya kitanzania hasa ukizingatia muongozo huo utatumika kuanzia ngazi za Wilaya mpaka Vijiji.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.